*************************’
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma Xaday amesema ziara ya siku moja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa kwenye jimbo lake imeleta mafanikio makubwa.
Mhandisi Hhayuma akizungumza baada ya ziara hiyo amesema imeleta mafanikio makubwa kwenye sekta ya afya na miundombinu.
Amesema wamepata nyongeza ya kilomita moja ya lami kwenye mji wa Katesh, hivyo mwaka wa fedha wa 22/23 zitajengwa kilomita mbili za lami.
“Ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya sh5.6 bilioni unaendelea, tumepata gari mbili za wagonjwa na nyongeza ya fedha ya kukarabati barabara ya Setchet-Hirbadaw- Zinga baada ya tathimini kufanyika,” amesema mhandisi Hhayuma.
Amesema pia utafanyika ujenzi wa barabara ya Waama-Diloda-Mureru kwa 33 kilomita 33 kwa mwaka huu wa fedha.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amesema ziara hiyo ya siku mbili ya Waziri Bashungwa imeendelea kwenye wilayani Mbulu.
Makongoro amesema akiwa wilayani Mbulu, Waziri Bashungwa atakagua miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu, afya, barabara na utawala kwenye Halmashauri mbili.
Amesema katika ziara hiyo Waziri Bashungwa ameambatana na Kaimu Katibu Mkuu Tamisemi Dk Charles Msonde.