…………………………
Na Mwandishi wetu.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini-THRDC umesema utaendelea kuwezesha Asasi za Kiraia, Watetezi wa haki za binadamu pamoja na wadau wengine wa haki kushiriki kutoa maoni katika hatua za awali za kuandaa Sheria mpya ya Chuo cha Mafunzo visiwani Zanzibar pamoja na ujengaji uwezo juu ya maswala ya Haki za binadamu kwa Maofisa wanaosimamia vyuo hivyo visiwani humo.
Imeelezwa kuwa mwongozo huo unatarajiwa kukamilka ndani ya wiki mbili zijazo na kukabidhiwa kwa uongozi wa Chuo cha Mafunzo kwa hatua zingine za kuukamilisha kwani tayari wanafunzi wamekuwa na matumaini makubwa na jitahada hizo za THRDC na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.
Hayo yamejiri kufuatia Waandishi wa Mwongozo huo Mratibu Taifa- THRDC Wakili Onesmo Olengurumwa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Magereza Zanzibar, Adv Seif Makungu kufanya ziara Katika baadhi ya vyuo vya mafunzo kwa ajili kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wanafunzi Wanawake, Wanaume pamoja na Watoto waliopo katika vyuo hivyo kulingana na uhitaji wao katika kulinda haki za bibaadamu.
Wamesistiza kuwa mwongozo huo umezingatia matakwa ya sheria za kimataifa pamoja na sheria za Zanzibar ili kuhakikisha mwongozo huu unaleta tija kubwa katika usimamizi wa vyuo vya mafunzo Zanzibar.
Imeelezwa kuwa Katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 13 na 14, takriban Wanafunzi 200 (wafungwa na mahabusu wamefikiwa) ambapo Kati ya hao wanawake ni 20, Watoto Wanaokinzana na Sheria 25 na Watu wazima 155.
Timu hiyo ya wadau wa haki wameweza kukusanya maoni kutoka asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu Unguja na Pemba tariban 50 ambao ni wanachama wa THRDC -Zanzibar.
“Lengo la kuwahusisha asasi hizo pamoja na wanafunizi wa vyuo vya mafuno ni ili kufanya mwongozo huu uwe umetokana na wahusika wenyewe ambao ndio watakuwa watumiaji wa mwongozo huu”Imeelezwa taarifa hiyo
Pia imesema Mwongozo huo umelenga kuboresha hali ya mawasiliano na utoaji taarifa za malalamiko katika njia ambazo sasa zitakuwa rasmi na zitakuwa zinasimimamiwa na magereza yenyewe kwa kushirikiana na wadau wa haki hapa Zanzibar.
Kwa Upande wa Wanafunzi na watetezi wa haki za binadamu wametoa maoni ya kuboresha mfumo huo na kutaka wahusika waukamilishe haraka na uanze mara moja kwani wanafunzi (wafungwa) wanamalalamiko mengi lakini hakuna njia za hara za kuziwasilisha.
Mbali na maoni na mapendekezo hayo wanafunzi (wafungwa) waligusia uhitaji wa kujua haki mbali mbali wanazostahiki wakiwa gerezani na kutoa malalamiko ya matukio na matokeo yanayotokea ndani ya magereza hizo ambayo ni kinyume na haki za binaadamu.
Wamefurahia mfumo huu na kuupongeza uongozi wa magereza Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Watetezi wa Haki za Binadamu Zanzibar kuja na mwongozo huu.
Timu ya wataalamu imefafanua kuwa mwongozo huu unaarajia kuleta suluhu ya kudumu hasa katika urahisishaji wa utoaji na upokeaji wa maoni kutoka kwa wanafunzi (Wafungwa) ambao mara nyingi hukosa huduma kwa wakati kutokana na kukosekana kwa mfumo rasmi unaowawezesha kutoa malalamiko, maoni au maombi yao kwa wahusika.
Hata hivyo Mfumo huo umeandaliwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo katika ya THRDC Zanzibar na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, mbali na uandaaji wa Mwongozo huu , pia THRDC Zanzibar wameanza mazunguzo ya kuandaa sera ya magereza pamoja na maboresho mengine ya msingi yatakayoweka mazingira wezeshi kwa Chuo cha Mafunzo Zanzibar kwenda na ulimwengu wa kisasa lakini pia kutoa haki stahiki na huduma kwa wanafunzi wa vyuo hivyo.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo Zanzibar ( Magereza), pamoja na wadau wa haki za binadamu kutoka vTume ya Haki za Binadamu Tanzania (THBUB), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jukwaa la Haki za mtoto Zanzibar (ZCRF), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) na Mahakama Kuu ya Zanzibar wamekamilisha mchakato wa kupokea maoni ya uboreshaji wa Rasimu ya Mwongozo wa Mawasiliano na Utoaji Malamiko ya Haki za Binadamu ( Communication and Complaints Guidelines) kwa wanafunzi (wafungwa) visiwani Zanzibar.
Ikumbukwe kuwa ziara hiyo imefanyika siku tatu kabla ya uzinduzi wa ofisi ya THRDC Zanzibar , ambao ulifanyika tarehe 17 Unguja Zanzibar katika Hotel ya Golden Tulip ambapo uzinduzi wa Repoti ya Mahitaji ya Mahakama Zanzibar pia ulizinduliwa na Mgeni Rasmi Katika shuguli hiyo alikuwa Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Mwinyi.