Tatizo la upatikanaji wa maji katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sasa litakuwa historia kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa uimarishaji mfumo wa kusambaza maji safi katika chuo hicho unaotarajiwa kukamilika mwaka huu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alipotembelea Chuo hicho.
Ndalichako amesema mradi huo unagharamiwa na mapato ya ndani ya Chuo hicho kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 na unalenga kutatua tatizo la mfumo uliokuwepo wa maji kushindwa kukidhi mahitaji ya wakazi katika Chuo hicho.
“Tumeamua kuboresha mazingira kwa vitendo na nimekuwa nikihimiza vyuo kutumia vizuri mapato yao ya ndani ili yatumike katika kazi za maendeleo kama hizi, sasa wakazi wa Chuo watapata maji wakati wote na tanki linalojengwa lina uwezo wa kuhifadhi maji yanayotosha kuhudumia wakazi kwa siku nne iwapo yatakatika,” amesema Waziri Ndalichako
Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Hellen Twigela ambae ni mhitimu wa UDSM hapohapo amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 500,000 ikiwa ni ongezeko la lita 455,000 ukilinganisha na lita 45,000 za sasa,ujenzi wa pampu ya kusukuma maji pamoja na ulazaji wa bomba jipya lenye urefu wa takribani kilomita 1.8.
Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye akizungumza katika ziara hiyo amesema chuo kiliamua kufanya mradi huo kwa kuwa kilikuwa na changamoto ya upungufu mkubwa wa maji na kwamba kazi hiyo iliyoanza Desemba mwaka 2018 inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu.
“Tayari kazi ya ujenzi wa tanki imekamilika na kazi ya ulazaji bomba inaendelea baada ya uchimbaji mitaro kukamilika hivyo kazi itakamilika kama ilivyopangwa,” amesema Profesa Anangisye.