Kijana wa Chipukizi, Mkoa wa Singida, Salumu Waziri akimvika Skafu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala mara baada ya kuwasili Ofisi ya CCM Mkoa wa Singida kwa ajili ya kuzindua Tamasha la Singida ya Kijani jana. Kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Dkt.Denis Nyiraha.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala akisalimiana na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu baada ya kuwasili mkoani humo.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aisharose Mattembe.
Baadhi ya Wabunge Mkoa wa Singida wakiwa kwenye kikao na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi (kushoto) akizungumza wakati wa kikao kifupi cha ndani na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala (wa pili kutoka kulia). Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Dkt.Denis Nyiraha.
Makada wa CCM wakiwa kwenye kikao hicho.
Wabunge, Elibariki Kingu wa Singida Magharibi (katikati) na Miraji Mtaturu wa Singida Mashariki (mapacha) wakimtuza Msanii wa kuigiza sauti za watu, Oscar Nyerere wakati akitoa burudani kwenye tamasha hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Dkt.Kitila Mkumbo akizungumza kwenye tamasha hilo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Singida (NEC), Yohana Msita akizungumza katika Tamasha hilo.
Tamasha likiendelea.
Tamasha likiendelea.
Mjumbe wa Baraza la UVCCM Taifa Mkoa wa Singida, Rehema Zombi akizungumza.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Dkt. Denis Nyiraha akimkabidhi keki maalumu ya tamasha hilo, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala.
Tamasha likiendelea. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Dkt.Kitila Mkumbo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida, Diana Chilolo na Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi.
Wana CCM wakiserebuka wakati Msanii Papi Kocha akitoa burudani.
Mwanamuziki Papi Kocha akipagawisha katika Tamasha hilo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba akizungumza.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala akihutubia.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala akiwa na baadhi ya wananchi waliojiunga na CCM wakitokea vyama vingine.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (mwenye miwani katikati nyuma) akiwa na baadhi ya Vijana wa CCM kutoka katika jimbo lake.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mwalimu Raymond Mwangwala amesema chama hicho kitaendelea kuongoza nchi hadi miaka 200 ijayo.
Mwangwala aliyasema hayo mjini hapa jana kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bashiru Ally wakati akizindua Tamasha la Singida ya Kijani lililofanyika viwanja vya Bombadier.
“Kutokana na chama chetu kuwa makini na kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu Dkt.John Magufuli ya kutekeleza miradi ya maendeleo CCM itaendelea kuongoza nchi hii hadi miaka 200 ijayo” alisema Mwangwala.
Alisema Rais Dkt.John Magufuli amefanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2015/ 2020 kwani hivi sasa elimu kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari inatolewa bure baada ya kusimamia matumizi mazuri ya fedha za serikali na kodi inayolipwa.
Alitaja maeneo mengine yaliyofanywa na serikali ni pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, reli, ununuaji wa ndege, barabara, umeme na sekta ya afya ambapo vituo vya afya, zahanati na hospitali zimejengwa nchi nzima akitolea mfano mkoani Singida ambako zimejengwa Hospitali mbili za wilaya ya Mkalama na Ilongero na vituo vya afya 11 vilivyogharimu zaidi ya sh.milioni 500 huko zahanati zikijengwa karibu vijiji vyote.
Mwangwala alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aisharose Mattembe kwa kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli katika sekta ya afya kwa kununua gari la wagonjwa lenye thamani ya sh.milioni 21 na vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Singida.
” Mbunge huyu hakika amefanya kazi kubwa ya kuwajali wanawake kwa kuwanunulia vifaa tiba hivyo vitanda vya wagonjwa 16 viwili vikiwa ni vya kujifungulia wajawazito vyote thamani yake ikiwa sh.milioni 11.6, kwa utendaji wake huu wa kazi ndio unaotakiwa kuigwa na viongozi wengine katika nchi hii” alisema Mwangwala.
Katika hatua nyingine Mwangwala aliwataka vijana wa CCM kuacha kukaa kimya badala yake wawajibu wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuitukana serikali na kuibeza nakueleza sasa iwe ni bampa tu bampa.
“Wewe kijana wa CCM popote pale ulipo ukiona mtu anaiponda serikali yetu mjibu papo hapo usisubiri hujibiwe na viongozi waliopo juu” alisema.
Alisema kumekuwa na maneno ya kejeri dhidi ya watu ambao wanajipendekeza na kumsifia Rais wetu ambapo alisema waendelee kumsifia ili wapate vyeo na kuachana na hao ambao wanashinda vijiweni wakilalamika.
Akizungumzia demokrasia aliyataka mataifa ya nje kutoingilia mambo yetu ya ndani na kuwa wao waendelee na yao na sisi watuache na demokrasia yetu.
Alisema katika uchaguzi ujao wa viongozi wa serikali za mitaa CCM itashinda kwa kiwango kikubwa kila maeneo na hii inatokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dkt.John Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Aliongeza kuwa hakuna kipindi cha wana CCM wanachojidai kama kipindi hiki cha uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli kwani majibu yote ya wananchi yamekwisha jibiwa.
Akizungumzia kuhusu tamasha la Singida ya Kijani lililoandaliwa na UVCCM Mkoa wa Singida alisema rangi hiyo ndio inawakilisha mambo yote mazuri na kuyakataa mabaya kama rushwa, uvivu, wizi na mengine mengi ambapo aliusifia mkoa huo kwa kuwa na ushirikiano baina ya viongozi wa serikali na wachama na kuwa ndio unaoongoza kwa kuwa na kura nyingi wakati wa uchaguzi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Dkt.Kitila Mkumbo akielezea kuhusu maji alisema serikali imetekeleza miradi mingi mikubwa ya maji nchi nzima na sasa inatarajia kutekeleza mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ambao umepitia shinyanga na kupelekwa makao makuu ya nchi Dodoma.
Katika Tamasha hilo viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wa CCM, Wabunge, Serikali na Wajumbe wa Baraza la UVCCM Taifa kutoka baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar walipata fursa ya kuelezea mambo mbalimbali ya maendeleo yaliyofanywa na kuendelea kufanywa na serikali.