SERIKALI inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari na wakati ukifika, wadau watajulishwa hatua inayofuata.
Ni kauli ya Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akitoa ufafanuzi kwa mwandishi wa habari aliyetaka kujua kuhusu maendeleo ya chakato wa mabadiliko ya sheria ya habari na hatua ulipofika.
Msigwa alisema, mapendekezo hayo bado yanapitia hatua mbalimbali na kwamba, serikali itatoa taarifa kwa wadau wa habari hatua inayofuata ikiwa ni baada ya kikao cha awali kilichokaliwa na wadau wa habari pia serikali tarehe 11-12 Agosti 2022.
“Serikali itatoa taarifa ni hatua ipi inayofuata, kwa sasa subirini lakini (mchakato) unakwenda vizuri,” Msigwa alimweleza mwandishi.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) tarehe 26 Agosti 2022, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alisema, serikali haitapeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari mpaka wadau wakubaliane.
Na kwamba, lengo ni kutengenesha sheria zenye maslahi kwa wanahabari na serikali lakini pia zitakazodumu kwa muda mrefu.