…………………..
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TBA jijini Dodoma. Miongoni mwa miradi iliyotembelewa inajumuisha mradi wa ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni B.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso amesema “leo tumefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TBA na kujionea namna miradi hiyo inavyotekelezwa.”
“Tumepata nafasi ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TBA ambapo tumeona kazi kubwa inafanyika ikiwa miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kuanzia eneo la Mji wa Serikali, Nzuguni B pamoja na Ikulu ya Chamwino. Jambo kubwa na zuri miradi hiyo inatekelezwa na vijana wengi wa Kitanzania” amesema Mhe. Kakoso.
Vile vile Mhe. Kakoso amesema kwa kasi ya utekelezaji wa miradi inayoendana nayo TBA kwa sasa, ni vyema Serikali wakauwezesha Wakala huo kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija kwa kuwa TBA inamilikia viwanja vingi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunaamini endapo Serikali itabeba jukumu la kuiwezesha TBA kwa kuipatia fedha za kuendeleza maeneo wanayoyamiliki ni imani yetu kama kamati kuwa Wakala huu utaweza kufanya uwekezaji mkubwa kwa kufanya ujenzi wa nyumba za makazi kwa Viongozi na Watumishi wa Umma. Vile vile TBA inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi ambapo tunaiomba Serikali kuhakikisha inaisidia TBA katika kuongeza kiwango kikubwa cha watumishi ili kuendana na mahitaji ya sasa” amesema Mhe. Kakoso.
Pia, Mhe. Kakoso ameitaka TBA kuwa na kiwanda cha kuzalisha kokoto ili kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi ili waweze kutekeleza miradi kwa gharama nafuu zaidi.
Aidha, Mhe. Kakoso ameipongeza TBA kwa kuendelea kufanya kazi nzuri katika maeneo ya ujenzi, usimamizi, ushauri na Ukarabati wa nyumba za viongozi na watumishi wa umma ambapo amesema kupitia ziara hiyo wameona kazi kubwa inayofanywa na Wakala huo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzu Sekta ya Ujenzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema amepokea maelekezo na mapendekezo ya Kamati hiyo hivyo kama Wizara watakwenda kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa TBA.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameishukuru kamati hiyo kuridhia kufanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na TBA na kuahidi kuongeza ubunifu zaidi katika miradi inayotekelezwa nchini.
“Leo tumepata fursa ya kutembelewa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambapo tumembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TBA hapa Dodoma. Nipende kusema kuwa tutayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ikiwa ni pamoja na kuwa na kiwanda cha kuzalisha kokoto ambacho kitasaidia kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi yetu. Pia nashukuru kwa pongezi zilizotolewa ambazo ni za TBA nchini nzima” amesema Arch. Kondoro.