CHAMA Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeiomba serikali kufanya mabadiliko katika sheria ya tozo za miamala ya kibenki ili kuepuka malipo mara mbili katika mishahara ya watumishi wa umma kwani inazidi kuwabebesha mzigo kwa familia zao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano (TALGWU) Shani Kibwasali amesema Suala la tozo linashughulikiwa kwa kushirikisha vyama vingine vya wafanyakazi kupitia TUCTA, ambapo serikali sikivu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilipokea maoni na mapendekezo ya vyama na imeahidi kulishughulikia.
Ameongeza kuwa watumishi wa umma kila mwezi wanalipa kodi kwa kukatwa katika mishahara yao. Lakini sasa kuanza kutekelezwa kwa sheria hii ya tozo inamfanya mtumishi wa umma kutozwa zaidi ya mara mbili katika pato moja kwa mwezi,” amesema Shani Kibwasali
“Niwaombe wanachama wetu tuendelee kuwa watulivu tukisubiri utekelezaji wake kwani tunaamini serikali yetu ni sikivu na suala hili litapatiwa ufumbuzi haraka,’.Amesema Kibwasali
Akielezea utekelezaji wa shughuli za chama hicho kwa kipindi cha nusu mwaka, amesema (TALGWU) imefanikiwa kushinda kesi 35 kati ya mashauri 39 yaliyokamilika katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, ambapo kulikuwa na mashauri 140 yaliyokuwa yakisikilizwa.
Amesema TALGWU kushinda kesi nyingi za wanachama kiasi hiki ni ushahidi tosha kwamba tunatekeleza jukumu la kuhakikisha haki inantendeka kwa wanachama wetu katika hatua za awali wakati mtuhumiwa anakamatwa,” alisema Kibwasali.
Awali, akitoa taarifa ya nusu mwaka kuhusu mafanikio waliyoyapata kwenye kutekeleza shugjhuli za chama, Kibwasali alisema nyongeza ya mishahara na kupanda madaraja kwa watumishi wa umma ni miongoni mwa mafanikio makubwa waliyoyapata kwa mwaka huu kwenye utendaji wa shughuli zao.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tukiishawishi serikali kutmiza takwa la kisheria na kanuni la kuwapandisha madaraja watumishi wa umma, hadi sasa suala hili limetekelezwa kwa asilimia 100, watumishi waliokuwa wamekwama kwenye nafasi moja kwa zaidi ya miaka sita sasa wamepandihwa madaraja.
“Pia serikali iliidhinisha Ikama na bajeti tatu ya mwaka 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022, utekelezaji huu umefanyika kwa kipindi cha Mei, Juni na Julai 2022 na katika utekelezaji huo jumla ya watumishi 56,000 wamepandihwa mishahara,” alisema.