Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Dkt. Rodrick Kisenge akiongea wakati akufungua rasmi Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiuetekelezaji lilofanyika MUHAS
Washiriki wa Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiuetekelezaji wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hilo
Mtaalamu Mwandamizi wa Afya, Sayansi za Kiutekelezaji, UNICEF, Dkt Robert Scherpbier, akieleza jinsi tafiti za kiutekelezaji zimeathiri utoaji wa program za UNICEF kwa washiriki wa Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiutekelezaji, MUHAS
Mkurugezi Mtendaji, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt Germana Leyna akichangia katika moja ya mada zilizowakilishwa kwenye Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiutekelezaji.
Kutoka kulia waliokaa ni Dr. Kasusu Klint, Mkuu wa Mradi wa CBHP MUHAS, Dkt James Kengia, Mratibu wa Timu za Usimamizi wa Afya za Mikoa, TAMISEMI, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Dkt. Rodrick Kisenge, Dkt Ulrika Baker, Meneja wa Afya, Huduma ya Afya ya Msingi, UNICEF na Dkt Robert Scherpbier, Mtaalamu Mwandamizi wa Afya, Sayansi za Kiutekelezaji, UNICEF kwenye picha ya pamoja na washiriki kutoka UNICEF pamoja na viongozi mbambali wa Serikali ikiwemo Wizara ya Afya na TAMISEMI
Washiriki wa Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiuetekelezaji katika picha ya pamoja katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
………………………………
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shikikishi Muhimbili (MUHAS) amesema kuwa Chuo kinaona fursa kubwa ya kuboresha zaidi utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania kupitia tafiti za kiutekelezaji.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi la Utafiti wa Kiuetekelezaji (Implementation Research), Makamu Mkuu wa Chuo aliyewakilishwa na Dkt Rodrick Kisenge, Mkurugenzi wa TEHAMA Chuo hicho amesema, MUHAS imeanza na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha ujumuishaji wa tafiti za kiutekelezaji katika programu mbalimbali na katika shughuli za kutunga sera za afya nchini.
Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa UNICEF – TANZANIA kiliandaa kongamano hilo lililojumuisha wadau kutoka UNICEF makao makuu na ofisi ya Tanzania, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na TAMISEMI, wanataaluma na wanafunzi wa MUHAS, na Taasisi zisizo za Kiserikali.Makamu Mkuu huyo wa Chuo alisema kuwa kwa sasa, MUHAS inafanya kazi kwa kushirikiana na UNICEF kuendeleza tafiti za kiutekelezaji nchini Tanzania.
“Kwa pamoja tunafanya tafiti za kiutekelezaji ndani ya programu chache zilizochaguliwa, na sasa tumeandaa kongamano hili linalolenga kuangazia mambo ya msingi na kuonyesha michakato ya utekelezaji wa utafiti kwa mifano hai kutoka kwa watafiti wa MUHAS”, aliongeza.
Tafiti za Kiutekelezaji ni aina ya tafiti za kisayansi ambazo hupambanua utendaji wa mikakati mbalimbali kwenye utoaji huduma kwa kuangalia kama inaendana na sera na uhalisia wa mazingira ambapo afua za kuboresha afya hufanyika. Mathalani katika afya, tafiti hizi hufanyika ili kujua endapo afua za afya au sera za afya zinatekelezeka, kutathmini utendaji na kupendekeza endapo imeonekana kuna mafanikio.
Baadhi ya afua za afya ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa kushirikiana na serikali ni pamoja na kuangalia namna muongozo mpya wa utendaji wa huduma zinazotolewa na wahudumu wa Afya ya Jamii unavyotekelezeka.
Pia tafiti zinaendelea katika kuangalia utekelezaji wa utoaji wa huduma za dharura kwa wajawazito kwa kuangalia afua ya mfumo wa bango kitita katika kuokoka maisha ya kina mama na watoto wachanga.