Wakati serikali ikijiandaa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi za Kimtandao, Wakili wa Kujitegemea James Marenga, amesema,ingependeza ahadi ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, kupeleka mapendekezo ya wadau wa habari katika bunge la mwezi huu (Septemba).
Wakili Marenga amesema hayo leo tarehe 8 Septemba 2022 ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Nape kusema ‘sheria’ hiyo imepata kibali hivyo Baraza la Mawaziri linatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria hiyo.
Wakati akifungua kongamano la siku mbili lililowakutanisha wadau mbalimbali wa Teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka nchi mbalimbali barani Afrika tarehe 7 Septemba 2022, Waziri Nape alisema muswada huo wa sheria unatarajiwa kuwasilishwa bungeni tarehe 13 Septemba mwaka huu.
Wakili Marenga amesema,wadau wa habari, wangependa kuona Waziri Nape anatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mapendekezo ya wadau kuhusu mabadiliko ya sheria za habari katika bunge la mwezi huu.
“Wadau wangependa kuoana ahadi ya Mh. Waziri Nape ya kupeleka Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge hili la mwezi Septemba mwaka huu ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike,” amesema Wakili Marenga.
Aidha Wakili Marenga amesema mjadala wa serikali na wadau wa Habari ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kwamba, kuna baadhi ya vipengele tayari wamekubakliana.
“Mjadala wa serikali na wadau ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016, na yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya wadau na yale ya serikali, kuna vipengele tulikubalia na vingine bado vipo kwenye mjadala,” amesema Marenga.
Akizungumzia sheria ya kulinda taarifa binafsi za kimtandao Wakili Marenga amesema, sheria hiyo si ya wadau wa habari pekee, inahusu watu wote.
“Halafu hii sheria ya data protection (ulinzi wa taarifa binafsi ) sio kwa ajili ya wadau wa habari pekee, ni sheria muhimu kwa watu wote,” amesema.