Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
OFISA Lishe Mkoani Pwani, Pamela Meena ameeleza hali ya lishe kwasasa kimkoa ambapo kuna asilimia 23.3 ya watoto wenye udumavu.
Aidha ameeleza, utoaji wa huduma ya matibabu ya utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano imeongezeka kutoka asilimia 82.3 kwa mwaka 2020/2021 hadi asilimia 103.4 mwaka 2021/2022.
Akitoa taarifa za utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya mkoa ,Pamela alieleza utekelezaji ni mzuri kwa mwaka 2021/2022 ukilinganisha na mwaka 2020/2021 .
Alieleza, viashiria vilivyotekelezwa vizuri ni utoaji wa fedha kwa 2021/2022 ambapo ni asilimia 84.42 ukilinganisha na mwaka 2020/2021 ilikuwa asilimia 67.5.
“Utoaji wa unasihi kwa wazazi/walezi wenye watoto chini ya miaka miwili imeongezeka kutoka asilimia 100 (2020/21) hadi 133.2(2021/22)”.
“Na utoaji wa vidonge vya nyongeza ya madini chuma kwa wajawazito imeongezeka kutoka asilimia 96(2020/2021) hadi 90.26(2021/2022)”;alifafanua Pamela.
Hata hivyo alielezea kwamba ,kimkoa wametekeleza viashiria vyote Tisa na kufikia malengo kwa ufanisi wa juu lakini katika baadhi ya Halmashauri ikiwemo Kibiti, Mkuranga, Bagamoyo na Rufiji havijatekelezwa ipasavyo kutokana na changamoto ya kutotoa fedha kwa wakati.
Pamela alisema, wamejiwekea mkakati wa kusimamia kutoa fedha kwa wakati ili viashiria viweze kutekelezwa kwa muda lengwa.
Mwenyekiti wa kikao hicho ,ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, aliwaeleza hataki kuona utekelezaji wa mkataba huo wa lishe unachezewa ,haitoshi kusema Kuna changamoto ya kuchelewa kutoa fedha kwa wakati huku viashiria vikikosa kutekelezwa kwa wakati.
“Kuchelewa kutoa fedha hiyo sio changamoto, huu ni udhaifu mkubwa kwa watendaji ,fedha zipo na mnashindwa kutoa kwa wakati kufanya utekelezaji” alisisitiza Kunenge.