Na.Abel Paul wa Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limefanya ukaguzi wa magari ya shule katika mkoa wa Arusha ambapo magari Zaidi ya mia moja na hamsini yamekaguliwa pamoja na kutoa elimu kwa wamiliki na madereva wanaoendesha magari hayo kutoka shule mbalimbali jijini Arusha.
Akiongoza zoezi hilo leo September 05 2022 mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha mrakibu wa Polisi SP Solomon Mwangamilo amesema zoezi hilo ni endelevu na wala sio hiyari ambapo amesema Jeshi la Polisi kikosi cha usalama Barabarani hakitosita kuchukua hatua staiki kwa mmiliki atakaye kaidi kuudhulia zoezi la ukaguzi wa magari ya shule.
Aidha SP Solomon Mwangamilo amesema sote tumeshuhudia namna vijana na Watoto wetu wanavyopoteza maisha katika ajali za magari haya ya shule, ambapo amesema ukaguzi huu na elimu kwa wamiliki na madereva utasaidia kupunguza ajali ambazo zimekatisha ndoto za vijana wetu ambao ni hazina kwa taifa.
Nao baadhi ya wamiliki wa shule waliojitokeza katika zoezi la ukaguzi wa magari yao wamelishukuru Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha hususani kikosi cha usalama barabarani kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa magari ya shule wa mara kwa mara ambapo wamesema kwa ambao wajafika kwa siku ya leo wajitokea kwani zoezi hilo ni rafiki na wanapata ushauri kutoka kwa wataalam.