…………………………..
Na Mwandishi Wetu
Wafanyakazi wa Banki ya CRDB tawi la TAZARA wametembelea Kiijiji cha Makumbusho na kufurahishwa na ujuzi wa ujenzi wa nyumba za asili za jamii mbalimbali za Tanzania.
Wafanyakazi hao wakiongozwa na Meneja wa Tawi, Bw. Elishumbo Mwasha wametembelea kituo hicho cha uhifadhi kama sehemu ya kuburudika na kujifunza juu ya mambo mbalimbali yanayofanyika Kijijini hapo.
‘Tumejifunza mambo mengi ambayo hatukujua kama yapo Kijiji cha Makumbusho ikiwemo teknolojia ya ujenzi wa nyumba za jamii mbalimbali ambapo kila mmoja wetu amefika na kujionea nyumba ya kijijini kwao.
Bw. Mwasha amesema kuna haja ya Watanzania kuwaleta watoto wao ili waweze kujifunza mambo mbalimbali pamoja na mila na desturi za jamii zao.
‘Nimefurahi sana kutembelea Kijiji cha Makumbusho nitawaleta watoto wangu wote waje kujifunza mila na desturi za kabila letu (Wachaga) ikiwa ni pamoja na jinsi babu zetu walivyoishi,” amesema Bw Mwasha.
Meneja wa CRDB Tawi la TAZARA ametoa wito kwa matawi mengine ya CRDB na taasisi zingine kutembelea Kijiji cha Makumbusho na vituo vingine vya Makumbusho ya Taifa ili waweze kujifunza mambo mbalimbali.
Naye Bibi Jane John alifurahia sana nyumba ya kwao (Waha) na kusema kuwa imemkumbusha nyumbani kwao Kigoma, aliingia ndani ya nyumba hiyo na kukaa chini huku akidai apigwe picha ya kumbukimbu.
‘Jamani nyumba hii imenikumbusha nyumbani kwetu Kigoma, nimefurahia sana uhifadhi huu,” alisema Bi Jane.
Kila mmoja wao alijisikia vizuri alipoiona nyumba iliyowakilisha jamii yao na kutokutamani muondoka katika maeneo hayo na kuahidi kurudi tena ili kujifunza zaidi.
Kijiji cha Makumbusho kilianzishwa mwaka 1966 kwa lengo la kuhifadhi ujuzi wa ujenzi wa nyumba za asili za jamii za Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Bw. Wilbard Lema amesema nyumba hizo katika Kijiji cha Makumbusho zinajengwa kwa mtindo wa kaya kwa kufuata ramani ya Tanzania na kwamba zinajengwa kwa kushirikiana na jamii husika
Bw. Lema ametoa wito kwa makabila mbalimbali nchini kujitokeza ili kujenga nyumba za makabila yao kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa.