Chama cha Act Wazalendo kimeiomba serikali, kuhakikisha kila Mtanzania anakua kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwawezesha Watanzania wote kupata bima ya afya ya Taifa.
Pia imeishauri serikali kupitia wizara ya fedha kuhakikisha mikopo yote inayodaiwa kupitia mashirika ya umma na Wizara kurudishwa ili kukipa uwezo mfuko wa bima ya afya kujiendesha wenyewe.
Rai hiyo imetolewa leo Dar es salaam na Msemaji wa sekta ya uwekezaji,Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii wa Chama hicho Mwanaisha Mndeme wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.
Pia Mwanaisha amesema kwamba serikali isimamie uwekezaji unaofanywa na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha unaleta tija katika mapato yake nakuuwezesha kuendelea kuwa himilivu.
” Act Wazalendo inaamini katika upatikanaji wa Bima ya afya kwa watanzania wote na hili tuliweka wazi katika Ilani yetu ya mwaka 2020 ni ahadi yetu wananchi wote tutaendelea kupigania upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wananchi wote bila kujali kipato chao” amesema
Aidha msemaji huyo wa sekta ya Uwekezaji,Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii wa Chama cha Act Wazalendo mesema kwamba kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya jumla ya Watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya Watanzania wote ( takribani milioni 59.4) ndoyo wananufaika na huduma za bima ya afya.
” Mfuko wa NHIF kwa sasa unahudumia wanachama 1,127,956 na wanufaika 4,341,993 sawa na asilimia 8 tu ya Watanzania wote huku asilimia 5.4 wanahudumiwa na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa ( CHF) asilimia 0.3 ya wanufaika wamejiunga kupitia SHIB- NSSF na asilimia 1 wanatumia bima za makampun binafsi kwahiyo asilimia 85.3 ya nguvu ya Watanzania haimo kwenye mfumo wa Bima ya Afya “amesema Mwanaisha.
Amesema kwamba Act Wazalendo inaimani kuwa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya matibabu kupitia huduma ya bima ya Afya kwa wote hivyo serikali inapaswa kuunganisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa kila mtanzania ili anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya afya moja kwa moja.
” Watanzania Waunganishwe na NSSF ili kupanua fao la matibabu kutoka idadi ya sasa asilimia moja ” amesema.