Mfamasia wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Neema Nagu akizungumza na wandishi WA habari Kando ya mkutano wa 10 wa kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2022/23 wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Mkutano huo umefanyika Kwa siku mbili Katika hoteli ya Golden Tulip Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Meneja Idara ya Majaribio na Usalama wa dawa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Bw. Mtani Njegere akizungumza Kwa. Upande wa udhiniti wa dawa Katika mkutano huo uliofanyika Kwa siku mbili Katika hoteli ya Golden Tulip Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Picha zikionesha washiriki mbalimbali wa mkutano huo uliofanyika Kwa siku mbili Katika hoteli ya Golden Tulip Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali wa afya ili kupata dawa za kutosha ambazo ni kingatiba na kuzisambaza katika jamii kwenye maeneo yaliyoathirika lengo ikiwa ni kuharibu mnyororo wa vimelea vinavyosababisha magonjwa yote yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo matende na mabusha, vikope, kichocho, minyoo na Usubi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Agosti 26, 2022) wakati wa mkutano wa 10 wa kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2022/23 wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Mfamasia wa mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Wizara ya Afya Bi. Neema Nagu amesema watahakikisha dawa hizo zina ubora unaostahili na salama kwa matumizi.
“Wizara itahakikisha dawa tunazozipata kwa wadau wetu, zina ubora unaostahili, salama kwa matumizi, na pale zinapoingia nchini tunazisambaza kwenda kwa maeneo yote yaliyoathirika ili jamii ipate na zitakapofika kwenye jamii zitolewe bila gharama yoyote kwasababu serikali imejipanga kuhakikisha magonjwa haya yanatokomezwa”
Aidha Nagu amesema dawa hizo zitawalenga hasa watoto wanaokwenda shule wenye umri kuanzia 5-14 na kwa jamii yote katika maeneo yaliyoathirika ili kuhakikisha kwamba wanapata kinga lakini pia kuua kabisa vimelea ndani ya mwili wa binadamu ambaye alishapatwa na magonjwa hayo ili asiendelee kusambaza.
Pia Nagu amesema Kila baada ya muda fulani wa kugawa dawa kwenye jamii, wizara huwa inapita kufanya tathmini ya kuangalia kama wanavyokwenda ni sahihi na mipango waliyoiweka.
“Kila baada ya muda fulani wa kugawa dawa , wizara huwa inapita kufanya tathmini ya kuangalia kama tunavyokwenda ni sahihi lakini pia kuchunguza kuona je yale maambukizi katika yale maeneo yamekwenda chini na kama hayajakwenda chini basi ni nini zaidi kifanyike kuhakikisha huo mnyororo wa usambazaji unakatika na maambukizi yanakwisha”
Nagu amuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba wizara itatekeleza yale aliyoyapanga kwamba kabla ya mwaka 2030 wanatokomeza magonjwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Mbali na hayo Nagu ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa Afya kuungana kwa pamoja na wizara ya Afya kutokomeza magonjwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, lakini pia wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wizara ya afya pindi inapokwenda kwaajili ya kusambaza kingatiba hizo kwa kuzitumia ipasavyo.
Kwa upande wake Meneja Idara ya Majaribio na Usalama wa dawa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) Bw. Mtani Njegere amesema Kwenye mkutano huo wao kama taasisi ambayo wajibu wake ni kusimamia udhibiti wa usalama na ubora wa bidhaa, wanahakikisha kwamba zile bidhaa ambazo zinatumika kutibu magonjwa ambayo yamesahaulika zinapoingia nchini kwamba ni dawa ambazo zinakidhi viwango vya ubora, ni salama lakini pia zina ufanisi.