Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu jimbo la Segerea jijini Dar es salaam Godlisten Malisa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi leo jijini Dar es salaam kuhusu muendelezo wa zoezi la sensa na makazi.
……………………
NA MUSSA KHALID
Vyombo la ulinzi na usalama vimeshauriwa kuimarisha ulinzi kwa watu wanaofanya kazi ya ukarani wa sensa wanapokwenda kuhesabu watanzania ili kuepukana na changamoto ya kuibiwa kwa vitendea kazi vyao.
Hayo yameelezwa leo na Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu jimbo la Segerea jijini Dar es salaam Godlisten Malisa wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kufuatia kuibuka kwa taarifa za wizi wa vitendea kazi vya makarani wa sense katika baadhi ya kata nchini.
Diwani Malisa amesema kuwa changamoto ambazo wamezibaini katika kata yake tangu kuanza zoezi la sensa kuwa ni pamoja na mtandao kuwa chini lakini pia vishikwambi kuisha chaji kwa haraka.
‘Licha ya changamoto hizo bado zoezi linakwenda vizuri na watu wameshafika kwenye kaya nyingi katika Kata yetu hivyo malengo yetu ni kuhakikisha tufanikisha zoezi hili muhimu sana kwa serikali’amesema Diwani Malisa
Aidha Diwani huyo amesema ili kuondokana na changamoto ya makarani kuibiwa kwa vishikwambi katika baadhi ya kata nchini ni vyema Jeshi la Polisi likaongeza ulinzi na usalama kwa makarani hao ili kuwadhibiti watu wasiopenda maendeleo ya nchi kufanikiwa.
Amesema ni vyema Jeshi la polisi likashirikiana na Polisi Jamii wa mitaa husika ili waweze kupewa ushirikiano wa kutosha kuingia katika maeneo yao na kutoa ulinzi kwa makarani.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa jiji la Dar es salaam wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema zoezi la sensa kwa mwaka huu limefanyika tofauti na nyuma kutokana na watu wengi kuhamasika zaidi.
Hata hivyo Diwani Malisa amewataka wananchi wa Kata ya Minazi Mirefu kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa makarani wa sensa ili waweze kufanikisha kwa wakati kazi waliyotumwa na serikali ili iweze kujua takwimu za wananchi wake.