********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Polisi katika nchi za Mashariki mwa Afrika waweke mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge yote ya uhalifu unaovuka mipaka ili wahalifu hao wasipate mahali salama pa kufanya uhalifu bila mkono wa dola kuwafikia.
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wadumishe ushirikiano baina yao ili waimarishe utendaji bila kujali mipaka ya nchi zao kwa sababu wahalifu wanatumia sana udhaifu wa kukosekana ushirikiano madhubuti miongoni mwa nchi hizo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 19) wakati akifunguaMkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), uliofanyika kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha. Amefungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema mfumo wa uhalifu duniani kwa sasa unachukua sura mpya kufuatia kukua kwa teknolojia hususani ya habari na mawasiliano, uhuru wa watu na bidhaa kuvuka mipaka pamoja na kuondolewa vikwazo vingi hususani visivyo vya kiforodha, hivyo kumewezesha kuwepo kwa fursa ya maendeleo kwani bidhaa na watu husafiri kwa wepesi na haraka zaidi hivyo kufanya ukanda huo na dunia kwa ujumla kuwa kama kijiji kimoja.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema maendeleo hayo kwa upande mwingine yameleta athari za kiusalama kwani wahalifu nao wanatumia fursa hiyo kuimarisha magenge yao ya uhalifu unaovuka mipaka, mfano biashara ya dawa za kulevya.
“Uhalifu mwingine ni wizi wa magari, ujangili, utoroshaji madini na biashaa haramu ya binadmu, ugaidi utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia na uharamia katika maziwa na baharini, utakatishaji wa pesa zinazotokana na uhalifu huo na vitendo vya rushwa.”
Waziri Mkuu amesema ushirikiano unahitajika katika kuzuia uhalifu ikiwemo mafunzo kwa watendaji hasa kwa makosa yanayovuka mipaka, operesheni za pamoja, upelelezi wa pamoja na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia ili kuyasaka, kuyabaini na kuyakamata magenge ya watuhumiwa wanaofanya makosa katika nchi moja na kwenda kujificha katika nchi nyingine.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kwamba anatambua katika jukumu lao la kutekeleza sheria bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili waweze kufikia lengo lao la kiutendaji kwa haraka zaidi.
Waziri Mkuu amezitaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na utashi wa kisiasa.“Ili kutokomeza uhalifu wa aina yoyote utashi wa kisiasa unahitajika sana. Lengo ni kuvipatia nguvu vyombo vya dola katika kusimamia sheria. Niwatake wanasiasa wengine tutoe ushirikiano kwa vyombo hivi ili viwe na meno kwa kutunga sheria zitakazo wawezesha kuafanya kazi zao ipasavyo”
Changamoto nyingine aliyoitaja Waziri Mkuu ni utofauti wa sheria baina ya nchi zao. Amesema iwapo sheria zao zitabaki kuwa tofauti, wataendelea kutoa mwanya kwa wahalifu. “Wahalifu wataendelea kufanya uhalifu nchi moja na kukimbilia nchi nyingine ambapo sheria haiwabani, lakini sheria zikiwa zinafanana watakosa pa kukimbilia.”
Waziri Mkuu amesema suala la vita dhidi ya rushwa lazima lisimamiwe kwa nguvu zote kwani kama hatua madhubuti hazitachukuliwa katika kuimarisha uadilifu, vitendo vya rushwa vitashamiri na kusababisha kuimarika kwa magenge ya uhalifu kwa vile wahalifu watakua na uhakika wa kukwepa mkondo wa sheria.
Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ustawi wa nchi zao katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii utategemea hali ya usalama, amani na utulivu, hivyo katika ukanda wao wa Afrika Mashariki wanategemea sana utekelezaji madhubuti wa mipango na mikakati watakayojiwekea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro ambaye leo amekabidhiwa uenyekiti wa EAPCCO, amesema atashirikiana vizuri na viongozi wenzake ili kuhakikisha hali ya amani na utulivu vinaendelea kuwepo kwenye nchi zao.
Pia, IGP Sirro ametumia fursa hiyo kuwashukuru marais wa nchi hizo kwa ushirikiano wanaowapa hali inayowawezesha kutimiza majukumu yao ipasavyo. Amekabidhiwa uwenyekiti wa shirikisho hilo na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Sudan na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika anayemaliza muda wake, Luteni Jenerali Adil Mohammed.
Shirikisho hilo linaundwa na nchi 14 ambzo ni Tanzania, Burundi, Jamuhuri ya Kimokrasi ya Congo (DRC), Djibouti, Kenya, Sudan, Sudan ya Kusini, Somalia, Rwanda, Uganda, Shelisheli, Comoro, Eritrea na Ethiopia.