Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akizungumza na waandishi wa habari Katika hoteli ya Hyyat Regency jijini Dar es salaam kuhusu mkutano wa Mabaraza ya Mawaziri wa maji bonde la mto Nile Leo Agosti 18, 2022.
Baadhi ya wapiga picha na waandishi wa habari wakimsimiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga wakati alipokuwa akizungumza Katika mkutano huo.
…………………………………….
Na Grace Semfuko,MAELEZO.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mikutano ya Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile iliyoanza Agosti 18-19 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Mikutano hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile katika kusimamia, kuendeleza na kutumia maji ya mto huo ambapo mkutano wa kwanza utakuwa wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchi za Mashariki (ENSAP) unaofanyika Agosti 18, ukifuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la mto nile (NILECOM) pamoja na mkutano wa Baraza Mawaziri wa Maji Ukanda wa Maziwa Makuu (NELCOM) itakayofanyika Agosti 19 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mhandisi Sanga amesema mikutano hiyo itatanguliwa na vikao vya kamati za Wataalamu kutoka nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile ambapo Tanzania pamoja na kuwa mwenyeji wa mikutano hiyo, pia itapokea uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la mto huo kwa mwaka 2022/2023 kutoka nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini.
*”Ili Dira ya pamoja , nchi zote za Bonde la Mto Nile zilianzisha program katika ukanda wa maziwa makuu- NELSAP kwenye mto White Nile, na Ukanda wa Mashariki- ENSAP kwenye Mto Blue Nile, na Tanzania ipo kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu- NELSAP, mikutano hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile katika kusimamia, kuendeleza na kutumia maji ya mto huo kupitia mipango mikakati na program za Bonde lake kama vile Mpango mkakati wa bonde la mti nile, wa mwaka 2017-2027, na program ya miaka mitano ya bonde la mto nile yaani Five Year Basin Wide Program”* Amesema Mhandisi Sanga.
Bonde la Mto Nile linahusisha nchi kumi za Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemikrasia ya Congo (DRC), Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini, Sudan, na Uganda ambapo nchi hizo zinasimamia na kuendeleza rasilimali za maji za bonde la mto huo chini ya mwavuli wa Taasisi ya mpito ya Nile Basin Initiative (NBI).