Kongamano likiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewakumbusha viongozi na wananchi
wa mkoa huo kutumia umakini,weledi, nguvu na akili kutekeleza zoezi la Sensa ya
Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Serukamba alitoa kauli hiyo leo Agosti 17, 2022 wakati akifungua kongamano la siku
moja la sensa ambalo limewahusisha , wabunge, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu Tawala,Makatibu Tarafa, madiwani kutoka kata zote 136, watendaji wa kata, viongozi wa CCM, viongozi wa dini na wajumbe wa kamati ya sensa ya mkoa.
“Napenda kuwakumbusha viongozi na wananchi wenzangu wa Singida kuwa
katika mambo ambayo tunapaswa kuyafanya kwa uaminifu, umakini, weledi na kutumià
nguvu na akili zetu zote kulitekeleza ni Sensa ya Watu na Makazi kwa sababu
ndiyo itakayotuletea huduma pale zisipokuwepo, kutuongezea na kuimarisha huduma
pale zilipo” alisema.
Alisema Serikali na wadau wa maendeleo hawaleti tu huduma kwa watu kwa kuwa
tu ni mafundi wa kusema bali ni kwa kutumia takwimu za idadi ya watu na
nyingine zitokanazo na tafiti mbalimbali zinazofanywa na ofisi ya takwimu.
Serukamba alisema hana mashaka na uwezo wa viongozi hao kwani
wamejidhihirisha tayari wao na umahiri wao kwa kila wakati kwa kupeana
majukumu.
” Nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu tangu zoezi la Sensa ya
majaribio kwa yale maeneo yaliyohusika hadi Zoezi la Anuani za Makazi”
alisema Serukamba.
Aliwata viongozi hao ambao ni wenyeji wa makarani wa Sensa katika maeneo
yao waende kufanya kazi kwa weledi ili kuitumikia nchi yetu kwa ufanisi wa
utendaji wa makarani wa Sensa ambao utategemea ushirikiano wao.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko alisema lengo la kongamano
hilo ni kutokana na umuhimu wa viongozi hao katika zoezi hilo na kuongeza nguvu
ya ziada ili kulifanikisha.
Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo , alisema Mkoa
wa Singida utakuwa na makalani na wasimamizi wa sensa 5,499 ambao watasimamia
zoezi hilo la sensa.
Alisema umuhimu wa Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi
zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,
mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za
maendeleo za kimataifa;
Taarifa za idadi ya watu husaidia
katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo
huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa
mgawanyo wa rasilimali.
Kipuyo alisema Mkoa wa Singida
umejipanga kufanya zoezi hilo kwa weledi mkubwa na kuwa mmoja wa mikoa
ambayo inatarajia kufanya vizuri baada ya wasimamizi na makarani hao kuwa
tayari kuifanya kazi hiyo kama walivyoelekezwa katika mafunzo waliyopata.