Naibu Spika Dr. Tulia Ackson amefanya uzinduzi wa chumba cha Computer kilichopewa jina la TULIA TRUST kilichopo katika Shule ya Sekondari Samora Machel iliyopo mkoani Mbeya ili kuwawezesha Wanafunzi kuweza kujifunza masomo ya computer kwa vitendo ili kuendana na teknolojia iliyopo sasa.
Awali Dr. Tulia aliwezesha shule hiyo kupata Computer tano za kuanzia ambapo pia ameahidi kuwaongezea Computer nyingine pamoja na mashine za kuchapisha mitihani na kutolea copy.
Katika hotuba yake Dr. Tulia amesema ”Kwakweli nimekutana na maajabu makubwa sana kwa hii hatua mliyofikia ya kujenga chumba hiki kizuri na kikubwa ingawa zimetajwa baadhi ya changamoto ikiwemo uchache wa Computer kwakuwa wanafunzi ni wengi, mimi niahidi tu kwamba nitaleta Computer nyingine hapa ili kuweza kumudu idadi ya wanafunzi”
“Nimeelezwa pia watoto wote hapa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita wanakaa mitaani ambapo ni changamoto kwao, kwenye hili niseme tutatafuta wadau na ikiwezekana tuanze kujenga mabweni kwa ajili ya watoto hawa lakini napenda tuanze na mabweni ya watoto wa kike kwasababu hawa changamoto zao ni kubwa zaidi ukilinganisha na wakiume ingawa tungetamani tujenge yote hivyo kwa kuanza tutaanzia hapo”-Dr. Tulia Ackson