Afisa Elimu Watu Wazima wa Wilaya ya Singida ambaye anashughulikia Afya, Anthony Kibuga (wa tatu kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi akipeana mikono na Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida, Parinemas Mashanjara katika hafla ya kukabidhiwa vyoo vilivyojengwa na shirika hilo iliyofanyika hivi karibuni katika shule ya Msingi Mwasauya iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Afesso Ogenga, Mratibu wa Miradi wa Shirika hilo, Violet Shaku na Mwenyekiti wa Kijiji cha Masauya, Justine Kidima.
Afisa Elimu Watu Wazima wa Wilaya ya Singida ambaye anashughulikia Afya, Anthony Kibuga, akizungumza katika hafla hiyo baada ya kukabidhiwa vyoo hivyo. |
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida, Parinemas Mashanjara akizungumza katika hafla hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI ya Austria kupitia Shirika la Sister Cities Salzburg –Singida
(SCSS) lililoko Salzburg Austria kwa kushirikiana na Shirika lisilokuwa la
Kiserikali la Community Initiatives Promotion (CIP) la mkoani Singida
limeendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua
sekta za elimu na afya nchini kupitia miradi mbalimbali inayofadhiliwa ambapo
limejenga vyoo viwili vyenye matundu 22 kwa thamani ya Sh.25 Milioni katika
Shule za Msingi ya Sokoine na Mwasauya zilizopo Halmashauri ya Wilaya Singida Vijijini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la CIP , Afesso Ogenga akikabidhi vyoo hivyo
alisema Ushirikiano wa maendeleo wa
mashirika hayo ulioanza tangu miaka 1980 ndio unaoendelea kutekeleza miradi
mingi ya kuchangia maendeleo kwa kiasi kikubwa ndani ya mkoa wa Singida.
Alisema makabidhiano ya vyoo hiyo
yameanzisha mchakato wa kihistoria ambayo italeta manufaa makubwa katika jamii
ya kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mradi huo ambao ni muhimu sana katika sekta ya elimu.
Ogenga alisema ili mwanafunzi aende shule ni lazima mazingira ya shule
husika yawe bora na rafiki na moja ya vitu muhimu ni kuwa
na mahali pa kujisitiri na kama hakuna huduma hiyo wanafunzi wanalazimika kwenda vichakani
au mbali zaidi kuifuata lakini inapokuwa karibu inawarahisishia kuhudhuria masomo na kuwapunguzia msongo wa mawazo wa
kufikiria mahali pa kwenda kujisitiri.
“Vyoo hivi ambavyo tunavikabidhi leo hii vimezingatia mahitaji ya watoto
maalum hasa wasichana, tunajua kwamba takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya
wasichana waliopevuka hawaji shule kwa sababu ya kukosa sehemu ya kujihifadhi
laikini katika vyoo hivi tumetenga eneo hilo jambo ambalo litawasaidia
kutositisha masomo” alisema Ogenga.
Alitaja jambo lingine kuwa vyoo hivyo vimejengwa kwa mfumo wa kisasa
vina maji ya kutosha ya kuflashi na sio vya shimo na kuwa ni bora zaidi kwa
matumizi kwani vinapunguza maambukizi ya magonjwa ya matumbo na UTI
ukililinganisha na vile vya shimo na hata kuvifanyia usafi inakuwa rahisi.
Alisema vyoo hivyo kwa kuvikadiria vitaweza kutumika hadi miaka 30 ijayo
ndio maana alisema makabidhiano hayo ynanakwenda kuweka historia hiyo ambayo
itaanzia kwa wanafunzi wanaoshuhudia tukio hilo na wale watakaokuja baadae na kusoma katika mazingira rafiki.
Mratibu wa Miradi wa
Shirika hilo, Violet Shaku awali ya yote alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wakazi wote wa Kata
ya Mwasauya, kwa muitikio wao katika kuchangia shughuli mbalimbali za
maendeleo, ambao kwa kiasi kikubwa umechangia katika ukuaji, utekelezaji na
mafanikio ya miradi ya maendeleo inayofanywa na Shirika la CIP.
Shaku alisema , shirika la CIP lilianzishwa mnamo mwaka 2002 lengo kuu
likiwa ni utoaji wa huduma kwa jamii zenye kiwango na
endelevu kiuchumi na kijamii kwa watu waliombali na huduma katika mkoa wa
Singida, kwa kuwaongezea uelewa, kuwajengea uwezo na utafutaji wa mali.
Alisema katika kutekeleza miradi hiyo shirika
hilo limejikita zaidi katika maeneo makuu matatu ambayo ni afya ambapo kwenye
afya tumekuwa tukitekeleza miradi ya kutoa mafunzo, kugawa vifaa tiba,
kufadhili wataalamu wetu kwa ngazi ya diploma na maswala ya boresha lishe
kupitia kwa wahudumu wetu wa afya ngazi ya jamii, tumejikita pia kwenye maswala
ya kuwainua kina mama kiuchumi kupitia miradi ya ufugaji kuku wa biashara na
mwisho kabisa ni elimu.
Alisema
katika kuunga mkono jitihada zinazo fanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika
kuleta maendeleo kwa wananchi, Shirika la CIP
linaendelea kujivunia kuwa miongoni mwa masharika yanayotia mkazo kwenye
swala la elimu shirikishi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
Akizungumzia
mradi huo uliotekelezwa katika shule hizo mbili alisema shirika limeweza
kujenga vyoo matundu 20 na vyumba vya faragha kwa wasichana viwili na kuweka
mifumo wa maji iliyogharimu kiasi cha sh 25,000,600. Vyoo hivi vimejengwa kwa
kushirikiana na uongozi na wananch katika kijiji cha Mwasauya. Ni vyoo
vinavyozingatia mahitaji ya watoto wa kike kwasababu vinatumia maji na hivyo
vinasaidia kupunguza magonjwa kama vile UTI na maradhi ya tumbo.
Shaku
alisema kwa miaka minne mfululizo
shirika limekuwa likiwajengea uwezo walimu 32 kutoka kata za Mwasauya na
Ikhanoda katika masomo ya hisabati na
kingereza, sambamba na hilo shirika limekuwa likisambaza vitabu vya kujifunzia
kwa wanafunzi wa kata hizi mbili, katika kuendelea kuwajengea uwezo walimu shirika
limekuwa likiwafadhili walimu kujiendeleza kimasomo kwa ngazi ya shahada na
stashada katika vyuo mbalimbali nchini ambapo mpaka sasa limefadhili walimu
wapatao wanne.
Aidha
Shaku alisema shirika hilo limetoa baiskeli 15 kwa ajili ya kuwasiadia
wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwasauya wanaoishi mbali na shule hiyo
ziweze kuwasaidia wakati wa kwenda shuleni na kurudi nyumbani ambapo awamu ya
kwanza zilikuwa tano na awamu ya pili 10.
Shaku
alitaja baadhi ya changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wa kutekeleza miradi hiyo kuwa ni
ongezeko la uhitaji wa huduma kuliko kile shirika linaweza kuhudumia,kukipokea
fedha kidogo kutoka kwa wahisani ambayo haiwezi kukidhi mahitaji yote ya wanchi
wetu.
“Leo
hii tunapokabidhi vyoo hivi, ni matarajio yetu kuwa ofisi yako, kwa kushirikiana
na viongozi wa chama na serikali pamoja na wananchi mtaunganisha nguvu katika
kutunza majengo haya na kufanyia ukarabati pale itakapohitajika” alisema Shaku.
Akizungumza wakati akikabidhiwa vyoo hivyo Afisa Elimu Watu Wazima wa
Wilaya ya Singida ambaye anashughulikia Afya, Anthony Kibuga ambaye alikuwa mgeni rasmi
alilishukuru shirika hilo kwa msaada mkubwa wanaoutoa katika wilaya hiyo kwa
zaidi ya maiaka 20 katika nyanja za elimu na afya.
“Binafsi kwa niaba ya Serikali tunawashukuru sana kwa kazi kubwa
mnayoifanya ya kuisaidia serikali katika maeneo yote mnayotusaidia” alisema
Kibuga.
Diwani wa Kata ya Mwasauya Salum
Juma alilishukuru shirika hilo kwa misaada hiyo inayoitoa katika maeneo hayo
hasa katika kata hiyo ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanufaika wa miradi
hiyo kuitunza na kuilinda huku akisisitiza kwa kusema msemo wa kiswahili usemao
kulea mimba sio kazi bali kulea mtoto akimaanisha kuwa kupata mradi ni kazi
moja na kuitunza ni kazi nyingine ambayo ndiyo ya muhimu sana.