Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari Leo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam kuhusu mkakati wa makusanyo ya Kodi mwaka 2022/23.
Na Zaituni Hussein, MAELEZO.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo, amesema mamlaka hiyo kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023, inatarajia kukusanya Shilingi Trilioni 23.65, ikiwa ni sehemu ya bajeti kuu ya Serikali ya Shilingi Trilioni 41.48, ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2021/2022, walikusanya kiasi cha shilingi Trilioni 22.99.
Bw. Kayombo amesema kufuatia ongezeko la makadirio ya makusanyo hayo, TRA inaendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa wafanyakazi na wafanyabiashara, ya kuhusu sheria mbalimbali za kodi, tozo na ada zilizofanyiwa marekebisho ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa sawa na kurahisisha ukusanyaji na ulipaji kodi kwa hiari na kutimiza majukumu na malengo yaliyowekwa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo amewataka watanzania kulipa kodi inavyostahili ili kujenga uchumi wa nchi.
*“Katika mwaka wa Fedha 2022/2023 tumeanza kwa kasi ya kuelimisha watumishi wetu na wafanyabiashara kote nchini juu ya mabadiliko mbalimbali ya sheria mbalimbali za kodi, tozo na ada zinazosimamiwa na TRA pamoja na taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali.”* Amesema Bw. Kayombo.
Aidha amebainisha kuwa, marekebisho na mabadiliko ya sheria za kodi yamefanyika kwa lengo la kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuimarisha sekta za uzalishaji kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi, ambapo miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na sheria ya usimamizi wa kodi ambayo inamtaka kila mwananchi mwenye Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
*“Katika mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa kodi, Sheria ya sasa inamtaka kila Mwananchi mwenye Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kusajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili kumwezesha katika shughuli zake za kila siku”.* Amesema Bw. Kayombo.
Amesema katika mwaka wa fedha uliopita wa 2021/2022, Mamlaka hiyo ilifanikiwa kutatua changamoto za walipakodi, kuweka mazingira mazuri ya kulipa kodi, kuongeza kasi ya kusajili walipakodi wapya, kuwekeza kwenye TEHAMA na kutoa elimu na kuhamasisha