WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara kwa kiwango cha lami zitatekelezwa, hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Mji wa Ifakara pamoja na wilaya ya Kilosa alipokuwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
“Kila alichokiahidi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli nitakisimamia kuhakikisha kinatekelezwa, hivyo wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu. Serikali yenu ipo makini na ina dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.”
Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli iko makini na inaendelea kuchapa kazi kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na mkoa wa Morogoro.
Pia, Waziri Mkuu alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini.
Waziri Mkuu alisema iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema watumishi wa umma wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu na maji. “ Sina mzaha na watakaotafuna fedha hizo.”