Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media, Bi. Nengida Johannes (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini leo tarehe 10, 2022 Dar es Salaam kuhusu Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Agosti 13 mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru, upande wa kulia ni Meneja wa Upendo Fm Radio Bi. Upendo JuherMeneja wa Uwanja wa Uhuru, Bi. Redenta Nyahonge akizungumza na waandishi wa habari jijini leo tarehe 10, 2022 Dar es Salaam kuhusu Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Agosti 13 mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media, Bi. Nengida Johannes (kushoto), Meneja wa Upendo Fm Radio Bi. Upendo Juheri wakionesha Tisheti zitakazovaliwa katika siku ya Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu litakalofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Agosti 13,2022.
……………………
NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Zaidi ya waimbaji wa nyimbo za Injili 20 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kupamba Tamasha la Vijana linalojulikana kwa jina la Twenz’etu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Agosti 13, 2022 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Tamasha hilo limeandaliwa na Upendo Media ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) kila mwaka ambapo washiriki watapata fursa ya kupata semina kutoka kwa wanenaji mbalimbali akiwemo Msaidizi wa Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Deogratius Masanya, Mkuu wa Mkoa Mstaafu Agery Mwanri.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 10/8/2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Upendo Media Bi. Neng’ida Johannes, amesema kuwa katika Tamasha hilo Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi ambaye atafungua Tamasha hilo.
Bi. Johannes amesema kuwa Tamasha hilo linafanyika kwa mwaka wa tisa tangu lilipoasisiwa mwaka 2014 na limekuwa likiwagusa vijana wa aina zote wenye imani zote.
“Tunatarajia kuwa na vijana zaidi ya 25,000 kutoka ndani ya Tanzania na nje ya nchi ikiwemo Rwanda, Kongo (DRC) pamoja na Uganda” amesema Bi. Johannes.
Amesema kuwa lengo ni kuwabadilisha vijana kwa na maadili mema kuhusu maisha yao na ambapo wanenaji watazungumza mambo mengi ikiwemo kuweza kujitegemea wenyewe na kuendesha maisha yao bila kuwa tegemeza.
Amebainisha kuwa waimbaji na kwaya mbalimbali zitakazotumbuiza katika Tamasha hilo ni Rehema Semfukwe, Hyper Squad, Yamungu Mengi (Komando wa Yesu), Kwaya ya AIC Chang’ombe, The Survivor Kwaya ya Efatha Morovian, Essence of Worship, Praise Team ya KKKT, DMP Jimbo la Magharibi.
Wengine ni Kwaya ya Vijana KKKT Usharika wa Vituka, Kwaya ya Uinjilisti Haleluya ya KKKT Usharika wa Mbezi Beach, Kwaya ya Vijana Mabibo Farasi, Kwaya ya Vijana KKKT Kitunda Relini na Kwaya ya Vijana KKKT Kinyamwezi
Hata hivyo amebainisha kuwa kuhusu usalama na Ulinzi wa siku hiyo jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke limejipanga kuhakikisha tamasha hilo linafanyika kwa amani na utulivu.
Amewataka vijana wote hapa nchini kuhudhuria tamasha hilo kwa kiingilio cha shilingi elfu tano (Sh 5,000) na tamasha hilo litaanza saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni.
Meneja wa Uwanja wa Uhuru, Bi. Redenta Nyahonge amewatoa hofu wananchi watakaohudhuria tamasha hilo kuwa kutakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha wakati wote wa tamasha hilo.
“Ulinzi umekamilika kila sehemu kila mageti kutakuwa na ulinzi wa kutosha, askali wa kutosha watakuwepo ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa” amesema Bi. Nyahonge.
Upendo Media wamekuwa waandaaji wa Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu mara tisa mfululizo likigusa maisha ya Vijana wa aina zote sio wakristo tu bali ni la watu wa imani zote, kwa mwaka huu kauli mbiu ya tamasha hilo ni WAZAMANI SI WA SASA.