Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji DK. Ashatu Kijaji akizungumza na wakuu wa mikoa na wilaya Nyanda za juu Kusini mkoani Mbeya Katika uzinduzi wa Royal Tour.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Amewaasa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri katika Mkoa wa Mbeya kuhusu kutumia vyema fursa ya utalii iliyofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour.
Waziri Dkt. Kijaji aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nyanda za juu kusini pamoja kuzindua Makala ya vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Mikoa iliyopo nyanda za juu kusini katika ukumbi wa Eden Highlands Hotel uliopo jijini Mbeya.
Dkt. Kijaji alisema kuwa serikali imetumia nguvu kubwa kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini kwetu lakini baadhi ya viongozi pamoja na watumishi walioko katika sekta ya utalii hutumia lugha isiyo faa kwa wageni hivyo kuwafanya wageni kutorudi tena kwa mara ya pili kuja kutalii nchini kwetu.
Awali Dtk kijaji alisema kuwa nchi yetu imejiwekea mkakati kupitia filamu ya ‘The Royal Tour’ kuwa na lengo la kuhakikisha idadi ya watalii wa nje na ndani ya nchi inaongezeka kutoka milioni 1.5 ambayo iliingizia taifa kiasi cha Dola ($) za kimarekani 2.4 milioni mwaka 2018 kabla ya kuibuka kwa janga la ugonjwa wa uviko 19 hadi kufikia watalii milioni 5 mwaka 2025 ambao inakadiriwa wataliingizia taifa kiasi cha Dola ($) za kimarekani Bilioni 6. Kwa muktadha huu, alitoa wito kwa wadau wa utalii waliohudhuria na ambao hawakuwepo, kuendelea kwa pamoja kuhamasisha filamu ya Royal Tour na kutangaza vivutio vilivyopo katika Mikoa saba ya Nyanda za juu kusini ambayo ni Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Katavi.