WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka washiriki wa kozi fupi ya 13 ya viongozi watambue, wafuate na waisimamie falsafa ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iliyojielekeza katika kuwahudumia watanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kuona mabadiliko ya kimtazamo, ushauri na maamuzi watakayoyafanya yanapaswa kuakisi walichokipata kupitia kozi hiyo mara baada ya viongozi hao kurudi kwenye maeneo yao ya utendaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 2, 2022) alipofungua kozi fupi ya 13 ya viongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Dar Es Salaam. Pia kozi hiyo itawaongezea uelewa na ufanisi katika eneo zima la ulinzi na stratejia kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kwamba washiriki wote, watatumia kikamilifu fursa hiyo adhimu kushiriki kwa umakini na uhodari wa hali ya juu ili kuongeza uelewa wao wa masuala mtambuka hususan ya kiulinzi, kiusalama na kistratejia.
Kozi hiyo inahudhuriwa na baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Waandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi za Kimkakati za Serikali.