Afisa Maendeleo ya Biashara mwandamizi NIC Bw. Nicholas Malakasuka akionesha maelezo mbaimbali yanayohusu bima ya mazao na mifugo katika banda la NIC kwenye maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye uwanja wa John Mwakngale jijini Mbeya leo.
Afisa Maendeleo ya Biashara mwandamizi NIC Bw. Nicholas Malakasuka akionesha maelezo mbaimbali yanayohusu bima ya mazao katika banda la NIC kwenye maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye uwanja wa John Mwakngale jijini Mbeya leo.
Wafugaji 379 wamekata Bima ya Mifugo katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) huku zaidi ya wakulima 1000 nao wakikata bima ya mazao ili kujiepusha na hasara inayoweza kuwakumba endapo watapata majanga mbalimbali katika shughuli zao na kilimo na ufugaji.
Hayo yameelezwa na Afisa Maendeleo ya Biashara mwandamizi (NIC) Bw. Nicholas Malakasuka wakati akizungumza na mtandao wa Fullshangwe katika banda la shirika hilo kwenye maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kwenye uwanja wa John Mwakngale jijini Mbeya leo.
Nicholas amefafanua kuwa wafugaji 25 kutoka Katesh mkoani Manyara, Wafugaji 189 kutoka West Kiliamnajro na karatu , Wafugaji 106 kutoka mikoa ya Singida na Dodoma ,Mkoa wa Simiyu wamekata bima za mifugo wafugaji 59 huku wakulima zaidi ya 1000 pia wakikata bima za mazao yao
Amefafanua kuwa NIC Haijaweka masharti yoyote kwa mtu anayejishughulisha na kilimo au ufugaji anaweza kukata bima katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) bila masharti yoyote na kufaidika na fidia pale anapopata janga lolote katika mazao yake iwe kuungua, Ukame, Mafuriko, Kuibiwa na kadhalika ikiwa ni pamoja na majanga yoyote yatakayotokea na kusababisha mifugo yake kufa au kuibiwa.
Ameongeza na kusema wakulima hawatakiwi kupata hasara katika shughuli zao za kilimo na kilimo kinatakiwa kilindwe ili kuleta tija na kuwafanya wakulima kunufaika na shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Aidha Bw. Nicholas amesema mkulima anaweza kulima shamba lake akapanda mazao lakini bahati mbaya yakatokea mafuriko yakasomba mazao yake hivyo mkulima kama amekata bima atatakiwa kuja kwetu na sisi tutafidia ile hasara iliyosababishwa na yale majanga kulingana na thamani ya bima yake.
Ameongeza kuwa kuna bima za kilimo za muda mrefu kama vile wakulima wa miti, mashamba ya kahawa na mazao mengine ya kudumu hawa watatakiwa kukata bima kila mwaka lakini mkulima wa msimu wale wanaolima mazao ya muda mfupi watatakiwa kukata bima zao za msimu tu.
Amewakaribisha wananchi mbalimbali kufika katika banda la (NIC) ili kujipatia bima za aina tofauti kama vile bima za magari, Bima za Maisha, Bima za Moto, zikiwemo hizo Bima za mazao na mifugo ili waweze kukata bima na kujiepusha na hasara ambazo zinaweza kuwapata mara baada ya kupatwa na majanga.