Ofisa Mkuu wa Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Yahya Charahani akitoa maelezo kwa baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya waliotembelea katika banda la Shirika hilo kwenye Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya katika maonesho ya Nanenane 2022 ambako Shirika hilo linashiriki.
Afisa Mkuu Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa, Bw. Emmanuel J. Lyimo akizungumza na mwananchi waliotembelea banda la maonesho la Shirika la Nyumba la Taifa mapema leo katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.
…………………………………………..
Mwandishi Wetu
Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) limebainisha mipango ya maendeleo ya ujenzi wa nyumba itakayowawezesha kuongeza wigo wa Watanzania kumiliki nyumba bora.Hayo yamebainishwa leo na Ofisa Mkuu wa Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Yahya Charahani wakati akitoa ufafanuzi kwa wateja mbalimbali ikiwamo Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya waliofika katika banda la maonyesho la Shirika hilo kwenye Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya kwenye maonesho ya Nanenane 2022 ambako Shirika hilo linashiriki.
Charahani amesema kuwa kwa sasa Shirika sasa linakuja kivingine likiwa limezingatia masuala muhimu katika ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi na hasa wa vipato vya kati na chini. Amesema kuwa hivi sasa linakusudia kuwa na sura halisi ya uongozi katika sekta ya nyumba kwa kutojenga tu nyumba bali pia kuongoza mipango muhimu ya kusukuma mbele ushawishi wa sera mbalimbali ikiwamo sera ya makazi na nyumba kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wadau.Pia amesema kuwa Shirika linaimarisha vitengo vyake kikiwamo cha huduma kwa wateja na masoko ikiwa niili viweze kujiwekea utaratibu wa kusikiliza maoni ya wateja na pia kuwatembelea wapangaji wake kwa lengo la kufahamu changamoto zinazowakabili katika nyumba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Mmoja wa Wateja hao Erhard Mlyasi kutoka Motisun Group amesema ni muhimu kwa Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha linachaziga katika utoaji wa elimu itakayowasukuma Watanzania kuishi kwenye makazi bora na yenye staha huku Shirika likisukuma mbele pamoja na wadau wengine suala la upungazji wa riba katika mikopo ya nyumba ili watanzania wengi zaidi wafaidike na nyumba.
Katika hatua nyingine amesema kuwa Shirika liko mbioni kutekeleza ujenzi wa majengo ya biashara ya Kashozi Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Mtanda mkoani Lindi, Kahama mkoani Shinyanga na Masasi mkoani Mtwara.”
Pia shirika litajenga nyumba za makazi Isofu mjini Sumbawanga na maghala ya mazao sehemu mbalimbali nchini, shirika litaendelea na mradi wa uuzaji viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara katika eneo la Safari City Arusha.
“Vile vile, shirika linatarajia kuanzisha viwanda vyake vya matofali, kokoto na mabati kwa ajili ya kupunguza gharama za ujenzi na kupata vifaa bora vya utekelezaji wa miradi yetu,”amefafanua Ofisa huyo.Maonesho hayo ya Nane Nane yamefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 1 Agosti 2022 yanafanyika katika Uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya.