……………….
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
USHIRIKIANO baina ya walimu wa michezo, wakuu wa shule na maafisa elimu umeiwezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ngazi ya Mkoa wa Dodoma ikizoa jumla ya vikombe vinane katika michezo mbalimbali.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokua akiongelea siri ya mafanikio ya timu yake katika kilele cha michezo ya UMISSETA ngazi ya Mkoa iliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Dodoma.
Mwalimu Rweyemamu alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tulijipanga vizuri. Mara tu baada ya kumaliza mashindano ya mwaka jana. Tulianza mikakati mapema kuanzia ngazi ya shule, tarafa na wilaya”.
Mkuu huyo wa Idara ya Elimu Sekondari alisema kuwa ushirikiano mkubwa baina ya walimu wa michezo, wakuu wa shule na maafisa ndiyo siri kubwa ya mafanikio kwa timu ya UMISSETA ya Jiji la Dodoma kufanya vizuri. “Wakati wa kufanya uchaguzi wa wanamichezo tulikuwa na umakini mkubwa. Tuliwachagua kwa uwezo wao na siyo kwa upendeleo. Tuliwatumia waamuzi wa nje wenye sifa kuchezesha na kufanya uchaguzi makini wa wanamichezo kwa lengo la kujenga timu imara na itakayotoa ushindani na kulinda hadhi ya Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Akifafanua ushindi huo wa kishindo, alisema kuwa timu hiyo ilipata jumla ya makombe manane. “Timu ya UMISSETA imepata makombe matano ya mshindi wa kwanza, makombe mawili ya msindi wa pili na kombe moja la mshindi wa jumla wa mashindano hayo” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Kwa upande wa mgeni rasmi ambae ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Aloyce Mwogofi alisema kuwa Mkoa wa Dodoma una imani kubwa na timu hiyo ya mkoa. “Sisi viongozi wa mkoa hatuna maneno mengi ya kusema, mengi mmeshaambiwa na viongozi wenu. Zingatieni taratibu za michezo hii, kwa jinsi nilivyowaona hapa nidhamu imetamalaki. Mkoa tunawatakia ushindi mkubwa, mlete jina la Dodoma kivingine” alisema Mwogofi.
Mashindano ya UMISSETA ngazi ya mkoa alihusisha michezo ya riadha, sanaa, usafi, mpira wa wavu na mpira wa mikono. Michezo mingine ni mpira wa kikapu, mpira wa pete na mpira wa miguu.