Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt Allan Kijazi wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika zoezi la usikilizwaji wa kero na malalamiko ya Ardhi kwa wananchi linaloendelea kufanyika kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Dar es salaam.
Kamishna wa Ardhi msaidizi Mkoa wa Dar es salaam Idrisa Kayera akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika zoezi la usikilizwaji wa kero na malalamiko ya Ardhi kwa wananchi linaloendelea kufanyika kwenye ofisi za Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika zoezi la usikilizwaji wa kero na malalamiko yao linaloendelea kufanyika kwenye ofisi za Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi jijini Dar es salaam(picha na Mussa Khalid).
…………………….
NA MUSSA KHALID
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria watendaji wote watakaobainika kuwa miongoni mwa chanzo cha migogoro ya ardhi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt Allan Kijazi wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika zoezi la usikilizwaji wa kero na malalamiko ya Ardhi kwa wananchi linalofanyika kwa wiki nzima kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Dar es salaam.
Dkt Kijazi amesema serikali haitakuwa tayari kuifumbia macho migororo yote inayohusu masuala ya ardhi kwani inakuwa na athari kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hivyo lengo lao ni kuhakikisha wanaibainisha na kuifanyika kazi kwa wakati.
Amesema kuna mambo makubwa yanayoathiri kuwepo na migoro ya ardhi ya mara kwa mara ikiwemo wanaanchi kutokuwa na uelewa wa sheria,kanuni na taratibu zinazoongoza masuala ya ardhi na hivyo kudhulumiwa haki zao.
‘Tumebaini kuna matatizo ya kiutendaji kwa watendaji wetu baadhi wamekuwa sio waaminifu na wamekuwa miongoni mwa wanaosababisha hii migogoro kuendelea kukua’amesema Dkt Kijazi
Awali akizungumza Kamishna wa Ardhi msaidizi Mkoa wa Dar es salaam Idrisa Kayera amesema mpaka sasa tangu kuanza kwa zoezi hilo la kusikiliza kero ya Ardhi kwa wananchi wameshasikilizwa zaidi ya 150 hivyo amewataka kuendelea kujitokeza zaidi ili kueleza changamoto zao.
Amesema zoezi hilo la kusikiliza kero linafanyika kwa siku nzima lengo ni kuhakikisha kuwa malalamiko yaliyokua yanaibuka mkoa wa Dar es salaam yanapataiwa ufumbuzi.
Amewasisi wananchi wote wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam kujitokeza kwa wingi kwani wanatekeleza Maelekezo waliyopewa na Rais Samia katika kutatua kero za wananchi.
Kwa Upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza Katika ofisi Hizo wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia viwanja vyao bila ya ufumbuzi hivyo wameiomba serikali kuwasaidia kuwatatulia changamoto zao bila ya kuwabagua.
Hata hivyo viongozi wametakiwa kuzielewa sheria za masuala ya ardhi na kuzitafsiri kwa njia sahihi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake bila usumbufu ambao sio wa lazima.