……………………
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa Jijini Arusha amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya Utalii nchini kwa lengo la kupokea maoni, kujadiliana namna ya kuiboresha zaidi Sekta ya Maliasili na Utalii nchini.
Waziri Balozi Dkt Chana amewapongeza wadau hao kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa huduma bora kwa watalii na akiwahakikishia kuwa Wizara anayoiongoza itaendekea kushirikiana nao ili malengo ya Serikali na ya Sekta binafsi yaweze kufikiwa kwa faida ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watoa Huduma za Utalii Tanzania ( TATO) Bw. Wilbard Chamburo amepongeza juhudi za Wizara za kukaa pamoja na wadau hao kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Amesema kuwa shirikisho hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya Utalii huku akieleza kuwa wakati wa Janga la UVIKO -19,TATO walikua mstari wa mbele kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya janga hilo kwa kutoa magari ya kubebea wagonjwa na kushiriki katika uanzishwaji wa vituo vya kupimia UVIKO 19 katika hifadhi za Taifa ikiwemo Serengeti.
Aidha, Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa TATO inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour ili kuhakikisha kuwa lengo lililowekwa la kufikisha watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 linafikiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania wanaojishughulisha na Biashara ya Utalii nchini (TLTO) Bw. Samuel Diah, amepongeza jitihada mbalimbali zinazo fanywa na Serikali katika kutatua kero zilizopo katika sekta ya Utalii akisisitiza kuwa hali hiyo inawatengenezea mazingira rafiki ya kufanya biashara .