…………………………
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake waendelee kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufasini katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Wanyamapoli, Misitu, Malikale na kuendeleza Utalii hapa nchini.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ametoa wito huo alipokuwa akifungua kikao kazi cha Menejimenti ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, Jijini Arusha chenye lengo la kujenga uelewa wa pamoja na kujadili utendaji kazi na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Wizara.
Waziri Balozi Dkt. Chana amesema kuwa kikao kazi hicho kitasaidia kuibua changamoto mbalimbali zinazo ikabili Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake na kuibua masuala muhimu yanayohitaji maamuzi ya pamoja katika kushughulikia kero mbalimbali kwa wananchi.
Kikao kazi hicho kinachoudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Eliamani Sedoyeka kinafanyika kwa muda wa siku mbili kikiwa na matarajio ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taasisi zake.