Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro akiangalia sehemu ya shehena ya ufuta uliokusanywa katika ghala la kijiji cha Molandi kata ya Marumba wilayani humo ambao utauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Marumba na Molandi wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro(hayupo pichani) alipokuwa katika ziara ya kuhimiza wakulima juu ya maandalizi ya msimu mpya wa zao la korosho ambapo amewataka kununua viuatilifu mapema kwa ajili ya kupulizia mashamba yao.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Marumba wilayani humo wakati wa ziara yake ya kuhimiza wananchi hususani wakulima wa korosho kuanza maandalizi ya msimu mpya wa zao hilo.
…………………….
WAKULIMA wa zao la ufuta katika kijiji cha Molandi kata ya Marumba wilayani Tunduru,wamehamasishwa kuendelea kuuza ufuta wao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuzingatia ubora ili waweze kupata fedha nyingi kutokana na zao hilo kuwa na soko kubwa Duniani.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro baada ya kutembelea zoezi la kukusanya ufuta wa wakulima katika ghala ya kijiji cha Molandi wilayani humo.
Amewataka wakulima,kuendelea kuzalisha kwa wingi kwa kuwa mahitaji ya zao hilo kwa sasa ni makubwa ikilinganisha na siku za nyuma kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukreni ambapo Mataifa mengi yanahitaji zao hilo.
“nimefanya ziara ya kukagua zoezi zima la upokeaji wa ufuta kwenye ghala la kijiji cha ambao unauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, nawaomba sana wananchi waendelee kukusanya ufuta wao na hawauzi nje ya mfumo huo ili waweze kunufaika na kazi wanayoifanya”alisema Mtatiro.
Aidha Mtatiro,amewaagiza viongozi wa serikali ya kijiji na kata kuhamasisha wananchi waokuchangia fedha na michango mingine kwa ajili ya ujenzi wa ghala kubwa,badala ya kuendelea kutumia ghala lililopo ambalo ni dogo na limeanza kuchakaa.
Amewataka viongozi hao kuwa wabunifu kwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na sio kutegemea michango ya viongozi na Serikali kwa kuwa tabia hiyo inaweza washindwe kufanikisha na kutekeleza mipango yao ya maendeleo.
“mimi sishindwi kuwaletea mifuko ya saruji ili kuendelea na ujenzi wa ghala lenu,lakini nahitaji mniletee mpango kazi wenu unaoonyesha mnahitaji nini,hii ni mara ya tatu nakuja kwenye ghala hili na naweza kurudi tena mara ya nne,sasa kwa utaratibu huu mlionayo hamtaweza kulijenga”alisema Mtatiro.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya alisema,zaidi ya tani elfu ishirini na tano(925,000) ya Dawa ya kupulizia korosho(Salphur)zimeanza kuwasili na kusambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Hata hivyo alisema, dawa hizo haziwezi kutosheleza kwa wakulima wote na kuwataka kuanza maandalizi ya msimu mpya kwa kununua Dawa kwa ajili ya mashamba yao huku wakisubiri utaratibu wa kupata viuatilifu vinavyotolewa na Serikali.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Said Manjolo alisema,wakulima wengi wanashindwa kuleta mazao yao kutokana na changamoto ya ghala ambalo kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ufuta limekuwa dogo.
Ameiomba Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru,kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa ghala jipya ambalo ujenzi wake ulianza tangu mwaka jana, lakini wameshindwa kuendelea kutokana na kukosa fedha ili wananchi wasiangaike kuhamisha mazao yao kupeleka maeneo mengine.
Manjolo, ameipongeza serikali kwa kusimamia na kuboresha mfumo wa uuzaji wa zao la ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeanza kuleta faida kubwa kwa wakulima.
Alisema, kwa sasa bei ya ufuta imeongezeka kutoka Sh.3000 katika mnada wa kwanza hadi kufikia Sh.3,040 bei ambayo haijawahi kutokea tangu waanze kulima zao hilo katika kijiji hicho.
Alisema,matarajio ya uzalishaji wa zao hilo mwaka huu ni makubwa zaidi kutokana na wakulima wengi kujitokeza kulima zao hila la biashara ambapo wanatarajia kuuza zaidi ya tani mia nne mwaka huu.
Mkulima wa zao hilo Said Hassan, ameishukuru na kuipongeza serikali kwa kuhamasisha,kuwapatia pembejeo kwa wakati na kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika la zao hilo.
“sisi wakulima tunaishukuru sana serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan kwa kutuhamasisha,kutupa elimu na mbegu na kuweka mazingira mazuri ya soko la ufuta”alisema.
Alisema,kutokana na mazingira mazuri hasa soko la uhakika ndiyo maana wananchi wengi wamehamasika kulima zao hilo na kuachana na kilimo cha baadhi ya mazao mengine ya biashara ambayo yalikuwa na changamoto nyingi katika uzalishaji wake.
MWISHO.