MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba, Meddie Kagere amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2019/20, huku Salum Mayanga wa timu ya Ruvu Shooting akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Kagere na Mayanga walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali, katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Kwa mwezi huo wa Agosti kila timu ilicheza mchezo mmoja, ambapo Kagere aliiongoza Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Ruvu, huku mshambuliaji huyo raia wa Rwanda akifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya goli.
Kagere aliwashinda Lucas Kikoti wa Namungo FC aliyefunga pia mabao mawili kwa timu yake katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda na Seif Karihe wa Lipuli aliyeiongoza timu yake kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo Karihe alitoa mchango mkubwa katika mchezo huo ikiwa ni pamoja na kufunga bao 1. Kagere na Karihe hawakupata kadi yoyote, wakati Kikoti alipata kadi ya njano.
Kwa upande wa Mayanga aliwashinda Mecky Mexime wa Kagera Sugar na Hitimana Thiery wa Namungo, ambapo aliiongoza Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Yanga moja ya timu vigogo hapa nchini na yenye wachezaji nyota wa ndani na nje ya Tanzania.
Mayanga aliwashinda Mecky Mexime wa Kagera Sugar aliyeiongoza pia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Biashara United, huku Hitimana Thiery ambaye aliyeipandisha daraja Namungo FC na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, ambapo katika mchezo wake wa kwanza wa ligi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Ndanda FC