Afisa Program kutoka Jukwaa la Utu wa Mtoto Marietta Mbunda akifanya mahojiani na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es salaam ikiwa ni katika kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa tar 16 Juni kila mwaka Afisa Mawasiliano kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea na kulinda haki za watoto (C-Sema) Faih Mkony akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es salaam ikiwa ni katika kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa tar 16 Juni kila mwaka.
………………….
NA MUSSA KHALID
Serikali na Asasi za Kiraia nchini zimekumbusha kubuni miradi mbalimbali ya kuiwezesha jamii kujikwamua kutoka kwenye umaskini na kuimarisha uchumi wa kaya badala ya kuwatumia watoto kama njia ya kupata pesa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Afisa Program kutoka Jukwaa la Utu wa Mtoto Marietta Mbunda wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi ikiwa ni katika kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa tar 16 Juni kila mwaka.
Afisa Program huyo amesema ili kukabilini na changamoto kwa watoto CDF imeratibu na kuanzisha Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania –TECMN kwa lengo la kuongeza upana wa mapambano ya ndoa za utotoni nchini Tanzania.
Mbunda amesema dhamira ya Mtandao huo ni kuhakikisha wanatokomeza ndoa za utotoni kwa kukuza uelewa juu ya athari katika jamii na kusimamia kukuza ustawi wa mtoto wa kike.
‘Kama tunavyojua siku ya mtoto wa Afrika inaadhimishwa kila ifikapo tar 16 Juni ya Kila mwaka na Tanzania ni moja ya nchi za afrika ambazo zimekuwa zikiadhimisha siku hii toka mwaka 1991 hivyo nasi kama mtandao lengo letu ni kuendelea kupasa sauti dhidi ya ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiendelea hasa kutilia mkazo kufanya mabadiliko ya sheria ya ndoa’amesema Mbunda
Kwa upande wake Faih Mkony Afisa Mawasiliano kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea na kulinda haki za watoto (C-Sema) amesema suala la ndoa za utotoni likekuwa ni changamoto kubwa kutokana na jamii kutokuwa na uelewa wa tatizo hilo.
Aidha Mkony ameyataja madhara ya ndoa za utoto kuwa ni pamoja na watoto kupoteza fursa ya elimu na ujuzi wa kazi,kupata maambukizi ya magonjwa,kuteseka Kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kutaka kujidhuru na kuongezeka kwa vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
‘Vilevile kuyumba kiuchumi na kudumu katika umaskini,kushindwa kujitawala na kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia’amesema Mkony
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu yanakwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa isemayo ‘Tuimarishe Ulinzi wa Mtoto,Tokomeza ukatili dhidi yake,jiandae kuhesabiwa’