Katibu mkuu wa chama Cha mapinduzi Daniel Chongolo kulia akiwa na viongozi wengine wa chama wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya uongozi
Baadhi ya vijana ambao wameshiriki katika mafunzo hayo ya siku kumi katika chuo hicho Cha Mwalimu Nyerere.
……………
Na Victor Masangu,Kibaha
VIONGOZI Vijana kutoka nchi rafiki za Kusini mwa Afrika wametakiwa kutumia mafunzo mbali mbali wanayoyapata katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ili kuweza kulinda maslahi ya nchi zao.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo wakati akifungua mafunzo ya awamu ya tatu ya Makada Vijana kutoka vyama rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Chongolo alisema kuwa makada hao vijana wanapaswa kutumia mafunzo hayo ya siku 10 kwa ajili ya kuwa viongozi bora wa chama na mataifa yao kwa kulinda maslahi na kuwaletea maendeleo wananchi.
“Makada Vijana mnapaswa kutumia mafunzo haya kwa ajili ya kujua na kutumia misingi ya ujamaa itikadi imani na falsafa za vyama vyenu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi huku wakilinda maslahi ya nchi,”alisema Chongolo.
Kwa upande wake Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Lubinga alisema kuwa chuo hicho kilijengwa baada ya Rais wa China kutembelea baadhi ya nchi rafiki mwaka 2012 na kukubaliana kujengwa Tanzania kwa ajili ya kuandaa vijana.
Lubinga alisema kuwa jiwe la msingi liliwekwa na Hayati John Magufuli mwaka 2018 ambapo Makatibu wakuu wote wa vyama hivyo rafiki walishiriki ambapo mafunzo hayo yanashirikisha makada Vijana 120 kutoka nchi hizo kupitia vyama hivyo.
Vijana hao wanatoka kwenye vyama vya CCM Tanzania, FRELIMO Msumbiji, MPLA Angola, ANC Afrika Kusini, ZANU PF Zimbabwe na SWAPO Namibia katika ugunguzi huo baadhi ya mabalozi wa nchi hizo na wawakilishi pamoja na viongozi waandamizi wa CCM na viongozi wa CCM kutoka Wilaya ya Kibaha na Mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge.