MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
BAADHI ya madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Pwani wameielekeza halmashauri hiyo kuangalia namna ya kuongeza mashine( posi )na mageti kwenye maeneo ambayo yanaonekana ni njia za panya zinazotumika kukwepa ushuru.
Hatua hiyo wameieleza ,inalenga kuinua mapato ya ndani ,kudhibiti utoroshaji na kudhibiti mianya ya wizi.
Wakizungumzia kwa nyakati tofauti, wakati wa baraza la madiwani, diwani wa kata ya Dutumi Mkali Kanusu na diwani wa Kilangalanga Mwajuma Denge walisema, yapo maeneo ambayo makusanyo yanashuka kutokana na kukosa posi na mengine watu kukwepa kulipa ushuru.
Denge alisema, kumekuwa na wimbi kubwa la kutorosha mkaa pasipo kulipia ushuru eneo la Ruvu Madimla kutokana na kutokuwepo geti.
Aliomba kwa mkurugenzi, kuweka geti pamoja na Mzenga Njiapanda ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Nae Kanusu alifafanua, suala la mapato ni la wote ambapo inastahili kusimamia wakusanyaji wa ushuru kwenye vizuizi na kuangalia namna ya kuongeza nguvu pasipo kuwepo mageti.
“Pia watendaji wa kata watoe taarifa ya makusanyo kwa madiwani,kutuambia kilichopatikana na changamoto zinazokwamisha kuongeza makusanyo,tubadilishe utaratibu wa kufanya tathmini wenyewe kuanzia kata,hii itatusaidia”alielezea Kanusu.