Waziri wa katiba na sheria Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza katika kikao cha wadau asasi za kiraia cha kuridhia na kupitisha mpango mkakati wa asasi hizo kuhusu utekelezaji wa maazimio 187 ambayo serikali iliyaridhia kati ya mapendekezo 252 kwenye mkutano wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa uliofanyika Machi mjini Geneva
Mbunge wa viti maalum kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania Bara NGOs Neema Lugangira hiyo katika kikao cha wadau asasi za kiraia cha kuridhia na kupitisha mpango mkakati wa asasi hizo kuhusu utekelezaji wa maazimio 187.
……………………….
NA MUSSA KHALID
Waziri wa katiba na sheria Dkt. Damas Ndumbaro amezitaka asasi za kiraia za watetezi wa haki za binadamu nchini kuzingatia Utanzania katika utoaji mapendekezo katika mapitio ya hali ya haki za binadamu.
Waziri Ndumbaro ametoa rai hiyo katika kikao cha wadau asasi za kiraia cha kuridhia na kupitisha mpango mkakati wa asasi hizo kuhusu utekelezaji wa maazimio 187 ambayo serikali iliyaridhia kati ya mapendekezo 252 kwenye mkutano wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa uliofanyika Machi mjini Geneva.
Dkt Ndumbaro amesema kuwa mapendekezo hayo yanalenga haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii ambayo Asasi za Kiraia zimejikita katika kukuza na kulinda haki za binadamu
‘Mapendekezo hayo 252 yalisambazwa kwa Wizara na Taasisi za Serikali, Mahakama, Bunge, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Asasi za Kiraia Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata maoni na maelekezo. Hivyo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikubali kutekeleza mapendekezo 187 kati ya 252 na kutoridhia kutekeleza mapendekezo 65. Hili ni ongezeko la idadi ya mapendezo ambayo nchi itayatekeleza kutoka maamuzi ya awali’amesema Dkt Ndumbaro
Aidha Waziri Ndumbaro amesema kuwa Mapendekezo ambayo Serikali imekubali kuyatekeleza ni yale ambayo yanaendana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sera, Sheria, Mikakati na Mipango ya Maendeleo ya nchi
Kwa upande wake mbunge viti maalum kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania Bara NGOs Neema Lugangira ameshauri asasi za kiraia kuendelea kutoa mapendekezo ikiwemo usawa wa kijinsia katika siasa.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki katika mkutano huo akiwemo Afisa Uchechemuzi Kituo cha Sheriana Haki za Binadamu LHRC Paul Kanegene pamoja na Afisa programu THRDC Perpetua Senkoro wamesema mkutano huo una dhumuni la kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji mapendekezo utakaofanya kazi kwa miaka minne ambapo baadae tathmini itafanyika kuangalia utekelezaji wake.
Baraza la haki za binadamu la umoja wa mataifa hufanya mikutano kwa kipindi maalum kufanya mapitio ya hali ya haki za binadamu kwa nchi wanachama ambapo nchi wanachama hutoa mapendekezo kwa nchi husika ambapo mwaka 2021 Tanzania ilishiriki na kupokea mapendekezo 252.