Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe amesema ataishawishi Wizara ya Fedha na Benki Kuu kuunda sera za kifedha ambazo zitakuwa rafiki kwa Wakulima na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.
Waziri Bashe amesema hayo kwenye mkutano na Wanahabari kuelezea maboresho ya huduma za Benki ya NMB zinazolenga kukuza Sekta ya Kilimo.
Aidha Mhe.Bashe ametoa shukrani kwa Benki ya NMB na Benki zote zilizoitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kushusha kiwango cha riba hadi kufikia asilimia 9 (Tarakimu moja) kutoka asilimia 21 (Tarakimu mbili).
Waziri Bashe ameipongeza Benki ya NMB kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ya chakula vijijini.
Waziri Bashe amesema hatua hiyo itawaepusha Wakulima na hasara inayotokana na upotevu wa mazao baada ya kuvuna mazao yao.
Awali; Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna amesema Benki hiyo imeshusha kiwango cha riba kwenye mikopo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi hadi kufikia asilimia tisa.
Bi. Zaipuna ameongeza kuwa NMB imetenga shilingi bilioni 120 zitakazokopeshwa kwenye Sekta ya Kilimo ambapo bilioni 20 zitaelekezwa kwenye ujenzi wa maghala na bilioni 100 zitaelekezwa kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na mnyororo wa thamani