Serikali imechukua hatua mbalimbali kupitia miradi inayofadhiliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika Visiwa vya Pemba na Unguja.
Hayo yamesemwa leo Septemba 5,2019 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akiwa Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Mwantum Dau Haji lililouliza kuwa kasi ya mmomonyoko wa ardhi na uhaba wa udongo katika Visiwa vya Unguja na Pemba vinatishia uhai wa visiwa hivyo. Je, ni hatua zipi za makusudi zimechukuliwa katika kuvinusuru visiwa hivyo?.
Mhe. Sima alisema kupitia Mradi wa Kujenga Uwezo wa Jamii Kuhimili Athari za Mabadiliko ya tabianchi-LDCF ambao umetekelezwa mwaka 2012 hadi 2018, shughuli mbalimbali zimefanyika zikiwemo ujenzi wa kuta mbili za mita 25 kila moja katika eneo la Kisiwa Panza-Pemba na ujenzi wa makinga bahari (groynes) matano ya wastani wa urefu wa mita 100 kila moja katika eneo la urefu wa mita 538 Kilimani-Unguja.
Pia Naibu Waziri alitaja upandaji mikoko Pemba maeneo ya Kisiwa Panza hekta 200, Tumbe hekta 10, Ukele hekta 7 na Tovuni hekta 1 na upandaji mikoko Unguja maeneo ya Kisakasaka hekta 8 na Kilimani hekta 1.4.
Aliongeza kuwa kupitia mradi wa Kupunguza Uharibifu wa Ardhi na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula katika maeneo kame nchini (2017-2022), shughuli zinazotegemewa kufanyika katika maeneo ya Micheweni Kata ya Micheweni na Kiuyu Maziwang’ombe ambazo ni kujenga makinga maji katika mashamba (dykes) ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba.
Nyingine ni kutoa elimu kuhusu kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mashamba darasa, upandaji wa miti ili kuhifadhi udongo na kutunza mazingira, na uanzishaji wa biashara ndogo ndogo ili kuwezesha jamii kuwa na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, kudhibiti mmomonyoko wa udongo, na kukabiliana na uhaba wa udongo. Alimalizia Waziri Sima.