Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha Vijijini
NAIBU Waziri ,ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia kazi , vijana na ajira Patrobas Katambi, ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya na Mikoa , kuingia mara moja katika ufuatiliaji na kuchunguza miradi iliyokutwa na dosari kubwa wakati Mwenge wa Uhuru ulipopita kwenye Maeneo Yao.
Aidha ameipa salamu mikoa na wilaya kutochukulia mzaha ukaguzi wa mbio za mwenge ,kwani Wizara na Serikali ipo kuhakikisha mwenge huo unatekeleza adhma na falsafa ya kuanzishwa kwake.
Akitoa maagizo hayo Shule ya msingi Mtongani ,Halmashauri ya wilaya ya Kibaha , Mkoani Pwani ,wakati alipojumuika kama Wizara yenye dhamana ya kuratibu mbio za Mwenge wa Uhuru aliitaka TAKUKURU kuchukua hatua ya haraka ili taratibu nyingine zifuate.
VILEVILE aliagiza, miradi iliyokutwa na kasoro ndogondogo kwenye mwenge na kutolewa maelekezo, Wizara inasihi Mamlaka zote katika Maeneo yanayohusika kufanya marekebisho haraka ili wananchi waweze kufaidika.
Naibu Waziri huyo aliziasa ,wilaya na mikoa ambazo bado hazijapitiwa na Mwenge kujiandaa na zihakikishe zinafuata maagizo wanayopewa .
Katambi aliwaasa ,kufuata maelekezo watakayopewa na kukubali kukusolewa na ambae atakaebainika kuikatisha tamaa timu ya vijana wakimbiza Mwenge Kitaifa hawata fumbiwa macho.
“Nawapongeza wakimbiza mwenge Kitaifa mnafanya kazi kubwa,hamlali,mpo kazini ,nawapongeza Sana;”
“Nipo hapa kwa niaba ya Waziri Mkuu, toeni ushirikiano kwa vijana Hawa sita,wameagizwa kufanya kazi na Rais Samia Suluhu Hassan, Hadi Sasa wameshafikia siku 36, wameshapitia miradi 284 yenye thamani ya sh.Bilioni 69.2”;! alifafanua Katambi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri alisema viongozi wa mbio za mwenge wapo vizuri katika ukaguzi.
Sara alisema ,vijana hao wanaofanya kazi kubwa na kwa mwendo huo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali.
Awali akipokea mwenge wa Uhuru kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Butamo Ndalahwa alisema Mwenge ukiwa Katika Halmashauri hiyo utatembelea miradi 12 yenye thamani ya Bilioni 2.2.
Butamo alitaja baadhi ya miradi inayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kuwa ni pamoja na , kuzindua madarasa ya sekondari Disunyara, kuweka jiwe la msingi Shule ya sekondari Kikongo, mradi wa maji MinaziMikinda,ujenzi wa kituo cha afya Kwala na kutembelea kiwanda cha Animal Care co.Ltd.
Kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa,Sahir Geraruma alieleza ,Mwenge Ni jicho la Rais kumulika utii wa sheria namna gani wananchi wanapewa huduma .
Alibainisha, unapita kukagua na kuhakikisha ubora wa miradi na thamani ya zinazotolewa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.