Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa huduma ya teleza kidijitali iliyo zinduliwa leo na Benki ya NMB, kampeni hii ni muunganiko wa huduma tatu ambazo ni Mshiko Fasta,NMB Pesa Wakala na malipo ya huduma kwa kutumia QR code. Kulia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango – Hamad Chande, wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede; kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) akifurahia baada ya kuzindua huduma ya teleza kidijitali iliyo zinduliwa leo na Benki ya NMB, kampeni hii ni muunganiko wa huduma tatu ambazo ni Mshiko Fasta,NMB Pesa Wakala na malipo ya huduma kwa kutumia QR code. Kulia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango – Hamad Chande, wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede; kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna.
**************************
BENKI ya NMB, imefanya mapinduzi makubwa ya kibenki ambapo imezindua huduma kubwa tatu kupitia kampeni yake ya Teleza Kidijitali zinazomwezesha mteja wa benki hiyo kupata mkopo kupitia simu ya mkononi bila kufika tawini na bila kuweka dhamana yoyote.
Huduma hizo zilizinduliwa leo katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Hafla hiyo pia ilishuhudiwa na Gavana wa Benki Kuu (BoT) Prof. Florens Luoga.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema kuwa huduma hizo zitaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kibenki nchini.
Aliitaja huduma ya kwanza kuwa ni mikopo kwa njia ya kidijitali ambayo NMB wameiita huduma ya MshikoFasta.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, huduma hii ya mikopo Kidijitali itamuwezesha Mteja wa Benki ya NMB kujipatia mkopo kwa uharaka na kwa urahisi kabisa kupitia simu yake ya mkononi bila kufika kwenye tawi lolote la Benki ya NMB na bila kuweka dhamana yoyote,” alisema na kuongeza.
“Huduma hii itapatikana kupitia NMB mkononi kwa simu za aina zote, simu janja (kwa App) ama kwa kutumia simu za kawaida (kwa kutumia USSD). Mteja wa Benki ya NMB, kwa kutumia huduma hii ataweza kukopa mpaka shilingi 500,000 ndani ya muda mfupi, kupitia simu yake ya mkononi,”
“Mheshimiwa Waziri Mkuu haya ni mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kibenki Tanzania na inaendelea tu kuthibitisha dhamira yetu ya kuendelea kuwa kinara katika mapinduzi ya huduma bora za kibenki na za kibunifu hapa nchini,” alisema.
Aliendelea kusema imezoeleka kuwa sehemu nyingi mabenki kutoa huduma zinazofanana na hii, kupitia mitandao ya simu, lakini kwa ubunifu waliokuja nao, wateja wa NMB watakopeshwa moja kwa moja na Benki na mikopo hii inaweza kurejeshwa ndani ya siku 1, siku 7, 14, 21 au siku 28.
Alisema riba ya mikopo hii itategemea kiwango kilichokopwa pamoja na muda utakaotumika kurejesha mkopo na mteja anapochukua mkopo, mtandao utaonyesha atarejesha Shilingi ngapi kwa muda aliouchagua.
Zaipuna alisema lengo la NMB ni kuhakikisha urahisi na uharaka wa kupata mikopo hususani kwa makundi ya wajasiriamali wadogo na wa kati, kama mama Ntilie, Bodaboda, machinga ambao wengi hawako kwenye mfumo rasmi kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi, kwa sababu ya aina za biashara zao, au kwa kukosa dhamana kwa ajili ya mikopo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, wiki iliyopita tulitembelea soko la wamachinga na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na tulijadili kwa kirefu maono makubwa aliyonayo Mkuu wa Mkoa kwa Wamachinga na wafanyabiashara wadogo, na ni furaha kwetu kuona kwamba kwa kutumia NMB MshikoFastatunakwenda kupunguza changamoto ya ugumu wa kupata mikopo na kuweza kusaidia kuongeza mitaji kwa makundi haya,” alisema
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kila kukicha shughuli za kibenki zinabadilika, na teknolojia imekuwa ndio chanzo kikubwa cha mabadiliko haya, hususani jinsi mabenki yanavyoweza kutoa huduma mbalimbali, kidigitali.
Sisi Benki ya NMB hatujabaki nyuma, tunaendelea kutumia rasilimali tulizonazo kuwekeza kwenye tekinolojia ili kuendelea kuleta masuluhisho kwenye jamii, kuendelea kuchagiza ukuaji wa teknolojia kwenye nchi yetu, na hivyo basi kuchangia katika ukuaji wa uchumi.”
Mtendaji huyo mkuu wa NMB, alitaja huduma ya pili iliyozinduliwa jana kuwa huduma ya NMB Pesa Wakala ambayo ni maboresho ya huduma ya NMB Wakala iliyopo sasa.
Alisema NMB Pesa Wakala, ni wakala atakayetumia simu yake ya mkononi kuwa Wakala wa Benki ya NMB na kuwezesha wateja wake kuweka na kutoa pesa kupitia simu zao za mkononi kama walivyo mawakala wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu.
“Kwa taarifa tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, Benki ya NMB tayari ina Mawakala zaidi ya 11,000. Kupitia huduma ya NMB Pesa Wakala, tunalenga kufikia idadi ya mawakala 100,000 nchi nzima ndani ya miaka mitano ijayo.,”
“Kikubwa zaidi, NMB Pesa Wakala sio tu itaenda kurahisisha huduma kwa wateja wa NMB, lakini pia ni sehemu ya kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania wenzetu. Ili kuwa Wakala wa NMB Pesa, sasa utahitaji tu simu yako ya mkononi, (simu janja (smart phones) au za kawaida maarufu kama ‘kitochi’), leseni ya biashara na kitambulisho cha Taifa,” alisema
Alitaja huduma ya tatu kuwa ni huduma ya Lipa Mkononi ambayo ni huduma ya malipo kwa njia ya QR code au Lipa namba.
Alisema huduma hii inawawezesha wafanyabiashara wakubwa na wadogo nchini kupokea malipo kwa njia za kidijitali ambapo linaruhusu kupokea malipo kirahisi, haraka na kwa usalama zaidi kutoka makampuni yote ya simu na mabenki ambayo yameunganishwa na mtandano wa Mastercard au VISA.
Alisema huduma hii itasaidia utunzaji fedha kwa wafanyabishara,na itaongeza usalama wa fedha zao maana hakuna haja ya kukaa na pesa taslimu au kupata usumbufu wa kutafuta chenji.
Alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa NMBitaendelea kuja na masuluhisho bora na nafuu kwa watanzania na uwajibikaji wao kwa jamii utabaki kuwa katika viwango vya juu
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dk. Edwin Mhende, alisema kuwa lengo NMB ni kuboresha na kurahisisha huduma zao na kuzifanya kuwa za kidigitali zaidi huku wakienda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia ulimwenguni na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa NMB (2020-2025).
Alisema NMB wanatambua umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya tehama kuwafikia na kuwajumuisha Watanzania wengi kwenye mfumo rasimi wa kifedha kwa maendeleo ya wananchii.
“Na sisi NMB, kwa kutumia vijana wetu makini ambao ndio chachu ya ubunifu huu tunaouzindua leo, tunajitahidi kukimbia mwendo sawa na maendeleo hayo katika Taifa letu na katika nchi za Bara la Afrika zilizopo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA).
Ni kwa msingi huo, leo hii NMB tunakuja na “TELEZA KIDIJITALI”, kampeni inayolenga kutoa elimu mahususi kuhusu mojawapo ya suluhishi mpya za kidigitali kutoka Benki ya NMB zinazo rahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza ulazima wa wateja wetu kufika kwenye matawi kupata huduma,”
Naye Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Luoga, aliipongeza NMB kwa kwenda na kasi ya maendeleo ya kidigitali na hasa kutumia vijana wao wa ndani kuanzisha huduma hizo.
Alisema uzinduzi wa huduma hizo kidigitali ni muhimu kwa jamii lakini pia inaonesha ushindani wa kibenki uliopo nchini.
Akizindua huduma hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema kuwa tukio lililofanywa na NMB kuzindua huduma hizo, inaonesha kuwa Benki hiyo ni kinara nchini.
“Yaani mtu anataka mkopo wa sh 300000, au 500000, haendi kwenye tawi lolote la benki, haonani na mtumishi yoyote wa Benki, atabaki kwenye simu yake, anaomba mkopo na anaupata, hayo ni mageuzi makubwa sana katika sekta ya kibenki,” alisema.
Alisema NMB kwa huduma hizo inakwenda kuchocchea maendeleo kwani wananchi wengi wataweza kupata mitaji ya mkopo wa riba nafuu na hivyo kuepukana na wajanja wanaotoa mikopo kwa riba kubwa.