Afisa wa Shirika la The Winamwanga Cultural Heritage Association (TWCHA), Veronica Kilango, akisoma risala mbele ya Afisa Mtendaji Kata ya Mzenga, Godfrey Ambelle kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya kilimo cha mkataba na ufugaji kwa vikundi 27 vilivyopo katika Tarafa ya Mzenga.
Wawakilishi wa wakulima ambao ni viongozi wa vikundi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Mratibu wa Mradi wa Shirika la The Winamwanga Cultural Heritage Association (TWCHA), Saidi Simkonda, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya kilimo cha mkataba na ufugaji kwa vikundi 27 vilivyopo katika Tarafa ya Mzenga vyenye wanachama 850 wilayani Kisarawe mkoani Pwani jana. Kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Mzenga, Godfrey Ambelle na Diwani wa Kata hiyo, Mohammed Rubondo.
Afisa wa Shirika la The Winamwanga Cultural Heritage Association (TWCHA), Veronica Kilango (kulia), akimkabidhi risala, Afisa Mtendaji Kata ya Mzenga, Godfrey Ambelle kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya kilimo cha mkataba na ufugaji kwa vikundi 27 vilivyopo katika Tarafa ya Mzenga.
Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Mzenga, Agness Msanya akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mwalimu Willbroad Rosper kutoka Taasisi ya Family Hope Foundation Tanzania (FAHOT), akiwa pamoja na Afisa Kilimo, Fatuma Kipingu katika hafla hiyo.
Afisa Mtendaji Kata ya Mzenga, Godfrey Ambelle kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, akizungumza.
Diwani wa Kata ya Mzenga, Mohammed Rubondo akizungumza.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, ambaye ni Afisa Tarafa ya Mzenga, Mulael Angelo akizungumza.
Afisa Ugani kutoka Kampuni ya Kilimo Joint, Joel Nchimbi akizungumza.
Mkulima wa Kata hiyo, Salum Kiame, akichangia jambo kwenye uzinduzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Kisarawe
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Shirika la The Winamwanga Cultural Heritage Association wameanza kutoa mafunzo ya kilimo cha mkataba na ufugaji kwa vikundi 27 vilivyopo katika Tarafa ya Mzenga vyenye wanachama 850.
Mafunzo hayo ya mwezi mmoja ambayo yameanza jana yatafanyika katika Kituo cha Agricuture Resouce Center kilichopo Kata ya Mzenga ambayo yatawakutanisha wadau wa kilimo wa wilaya hiyo wakiwemo wawakilishi wa vikundi vya wakulima, watengenezaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo, Taasisi za kifedha pamoja na wanunuzi wakubwa wa mazao.
Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Mratibu wa Mradi wa shirika hilo, Saidi Simkonda alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wakulima wa kujua mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali zitokanazo na kilimo ili kufanya kilimo chenye tija.
Simkonda aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine Bodi ya shirika hilo ilikaa na kuona ni bora kuwa na leseni ya biashara ili shirika liweze kuanza kununua mazao ya wakulima wake kwa wakati ili kufanya kilimo cha mkataba kiwe cha moja kwa moja ambapo Halmashauri ya wilaya hiyo imetoa leseni ya biashara kwa shirika hilo yenye namba B.2874206.
Mratibu huyo alitaja mafanikio waliyopata katika kufanikisha kilimo hicho cha mkataba kuwa ni kupata ardhi yenye ekari 50 toka Serikali ya Kijiji cha Gwata kwa ajili ya kuwekeza kiwanda cha kusindika nafaka na kutoa unga wa mahindi chenye uwezo wa kusindika tani 20 kwa masaa 24 kupitia mtambo wenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni mia moja na kumi na mbili za kitanzania kutoka Kampuni ya Shijia Nhuang Hongdefa Machinery Comp Ltd ya Nchini China.
Afisa Mtendaji Kata ya Mzenga, Godfrey Ambelle akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo, alisema elimu watakayoipata ndiyo itakayopelekea kuwatoa katika dimbwi la umaskini kupitia kilimo hicho cha mkataba na kuwa kinachohitajika ni soko la uhakika wa mazao ya wakulima.