………………………
Adeladius Makwega-DODOMA
Watanzania wametakiwa kutimiza ahadi mbalimbali wanazitoa katika maisha yao, ni heri kutoitamka hadharani kuliko kuitoa alafu kushindwa kuitekeleza.
Kauli hiyo imetolewa na Padri Paul Mapalala paroko wa parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma katika misa ya Jumapili ya Machi 13, 2022 parokiani hapo.
“Kulikuwa na mgonjwa mmoja maututi alikuwa katika foleni ya kumuona daktari bingwa mgonjwa huyu alifika hapo kwa kubebwa machela, wagonjwa wengine walimuonea huruma wakasema ndugu yetu huyu asikae foleni. Akaruhusiwa moja kwa moja kumuona daktari. Alipatiwa huduma na akapata nafuu kiasi. Akiwa hapo wodini alitamka kwa manesi na madaktari kuwa anawaomba watumie kila namna apone, wakifanikisha hilo atatoa mamilioni ya fedha zake kwa ajili ya kuboresha hospitali hiyo.”
Baada ya juma moja mgonjwa alipona na kurudi zake nyumbani kwake, huku ahadi aliyoitoa hakuitimiza na hata alipoulizwa na wahudumu hawa wa afya aling’aka mno. Jamani timizeni ahadi zenu iwe kwenye familia na hata katika jumuiya zetu, alisema Padri Mapalala.
Misa hiyo ya pili parokiani Chamwino Ikulu pia iliombea mvua kunyesha kwa ajili ya mazao mbalimbali yaliyopandwa mashambani.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia Alizeti, Karanga Kunde Maboga na Mahindi mashambani yakiwa ya rangi ya Chanikiwiti, huku mahindi yakianza kutoa mbelewele.
Kwa juma moja eneo la Chamwino Ikulu halikujaliwa kupata mvua, huku jua kali likiwaka.