Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) pamoja na viongozi na wataalamu wengine wakitoka katika jengo la Maabara la hospitali ya Wilaya ya Nkasi.
mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ( wa Mbele) akikagua jengo la Utawala katika Hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga iliyoko katika Kata ya Mtowisa, bonde la ziwa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ( wa pili toka kulia) akiongozana akiongozana na Karani wa Mradi wa ujenzi wa Chuo Cha Ufundi VETA Mkoani Rukwa Mhandisi Jeremiah Longido wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa chuo hicho.
Baadhi ya majengo ya Chuo Cha Ufundi VETA Mkoani Rukwa.
**************
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Tender International kuhakikisha anamaliza ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA kilichopo Kata ya Sumbawanga Wenyeji Wilayani Sumbawanga ndani ya mwaka huu ili kufikia mwezi Januari mwaka 2020 kianze kudahili wanafunzi katika fani mbalimbali za ufundi.
Chuo hicho ambacho ujenzi wake ulitakiwa kumalizika Septemba 21, 2019 bado haujakamilika kutokana na Mkandarasi huyo kutegemea fedha za ujenzi kutoka serikalini na hivyo kuomba kuongezewa muda wa miezi minne ili aweze kumalizia ambapo hadi sasa ameshalipwa shilingi bilioni 2.6 kwaajili ya ujenzi wa majengo 22 ikiwemo karakana mbalimbali za mafunzo, mabweni, madarasa na nyumba za watumishi.
Mbali na changamoto hiyo Mh. Wangabo pia amepongeza kiwango cha ubora wa majengo hayo ambayo kwasasa yapo katika hatua ya kupauliwa na kuongeza kuwa kama kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imeridhishwa na kiwango cha majengo ya chuo hicho hadi hapo kilipofikia.
“VETA hii ilianza kujengwa mwaka jana mwezi wa tisa na ilitegemewa iwe imemalizika mwaka huu, kipindi cha mwaka mmoja. Lakini kumekuwa na changamoto za hapa na pale upande wa mkandarasi n ahata upande wa wizara inayohusika, basi hizi changamoto zimefikia kwenye hatua ambayo sasa tunaweza kwenda vizuri, Mkandarasi ameomba kuongezewa miezi minne na hii mimi nitaifuatilia, kuhakikisha kwamba hii ‘extention’ inakwenda haraka ili ikamilike ili ianze kuchukua wananfunzi Januari 2020,” Alisema.
Ameyasema hayo leo tarehe 29.8.2019 alipotembelea katika eneo la Ujenzi wa Chuo hicho kinachotarajiwa kudahili wanafunzi 600 wa masomo ya muda mrefu na wanafunzi 2000 wa masomo ya muda mfupi katika fani za umeme wa majumbani, umeme wa magari, ushonaji, mapishi, ufundi wa kompyuta, ufundi wa magari, useremala, na usindikaji wa chakula.
Awali akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya ujenzi wa Chuo hicho karani wa Mradi Mhandisi Jeremiah Longido alisema kuwa endapo serikali italipa fedha za ujenzi kwa wakati wana uhakika kwamba majengo hayo yatakamilika katika kipindi hicho cha miezi minne waliyoiomba na hatimae kufikia mwezi January, 2020 kuanza kudahili wanafunzi.
“Kama ‘Cash flow’ itakwenda vizuri, hii miezi minne kama kazi itafanyika kwa nguvu tunaweza kumaliza kazi, kwasababi amelipwa ‘certificate’ namba nne ambayo ni kama milioni 130 lakini kuna ‘certificate’ namba tano kama milioni 640 amabyo ipo tayari ambapo mda wowote anaweza kulipwa kwahiyo kama hiyo atapokea inamaanisha tutakuwa vizuri,” Alisema.
Katika Hatua nyingine, Mh. Wangabo amesikitishwa na kasi ya konokono katika ujenzi wa hospitali za Wilaya ambazo kwa mujinbu wa tarehe za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, hospitali hizo ziliongezewa muda wa kuisha kwake na zilitakiwa kumalizika na kukabidhiwa tarehe 31.8.2019 kwaajili ya kuanza kutumika.
“Kasi yenu ni ndogo, kasi ya konokono, vifaa havipo hata ujenzi katika jengo hili la utawala hakuna, hali kwakweli ni hovyo na si nzuri ni mbaya muda umekwishaisha, kwahiyo nashindwa hata kuwaambia kuna siku za nyongeza kwasababu kuna ‘deadline’ ya TAMISEMI. Sasa fanyeni juu chini kwa siku zilizobakia mmalize hapa sasa sijui mtaweka hema ama mtafanyaje lakini fanyeni juu chini hii kazi iishe,” Alisisitiza
Ameyasema hayo baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, viongozi na wataalamu wa wilaya ya Sumbawanga ambapo kabla ya kufika hapo pia alitembelea hospitali ya Wilaya ya Nkasi na hospitali ya Wilaya ya Kalambo.