Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la baraza la wawakilishi Zanzibar, Dkt.Mohammed Said akizungumza na Wanahabari baada ya kutembelea Maabara za TMDA na kushuhudia shughuli ambazo zinafanywa na Mamlaka hiyo
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile akipata picha ya pamoja na wajumbe Kamati ya ya Bajeti Bunge la wawakilishi Zanzibar baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile akizungumza na Wanahabari baada ya kuwapokea Wajumbe wa Kamati ya ya Bajeti Bunge la wawakilishi Zanzibar baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)
****************
NA EMMANUEL MBATILO
Dkt.Ndungulile amewahakikishia wananchi kuwa dawa zote zinazotumika hapa nchini ni salama kwani kuna maabara ya kisasa inayoshughulika kufanya uchunguzi wa dawa na vifaa Tiba kabla havijaingia katika matumizi kwenye jamii.
Ameyasema hayo leo Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile baada ya kuwapokea wajumbe Kamati ya ya Bajeti Bunge la wawakilishi Zanzibar baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha Wanahabari pamoja na Wajumbe wa Kamati hiyo Mh.Ndungulile amesema kuwa wananchi hawapswi kuwa na mashaka ya dawa zinazouzwa katika maduka kwa sababu maabara ya TMDA inaongoza kwa ubora ndani ya bara la Afrika na wako katika mkakati wa kuomba kibali cha kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani(WHO).
“Niwaombe wananchi kutosambaz taarifa ambazo hawana uhakika nazo, kama wana swali au hoja kuhusu ubora wa dawa ni bora wawasiliane na TMDA kwa sababu sasa tutaanza kuchukua hatua kwa sababu ni upotoshaji usiokuwa na msingi.” Amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amewataka kamati hiyo kuwa mabalozi wazuri Zanzibar hasa kutokana na kujifunza na kuona shughuli zinavyofanywa na TMDA.
“Maabara yetu imekuwa ni mfano hasa nchi nyingi zimekuwa zikija kujifunza kwetu pamoja na hayo wananchi wanatakiwa kuzingatia misingi ya matumizi ya dawa, watu wasinywe dawa pasipokuandikiwa na daktari”. Amesema Dkt.Ndugulile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la baraza la wawakilishi Zanzibar, Dkt.Mohammed Said amesema kuwa wamejifunza mambo mengi kwa wenzao TMDA hivyo na wao wanaweza kuimarisha kitengo chao cha ZFDA ili kuona wanaweza kufanya uchunguzi wa mambo mbalimbali.
“Tumekuja kuona wenzetu wanafanyaje ili nasi tuweze kuishauri serikali yetu kutenga bajeti kubwa kwa ZFDA kuona tunanunua mashine nzuri pamoja na kuzifanya maabara zetu kuwa za uhakika”. Amesema Dkt.Said.