Home Mchanganyiko TAKUKURU YAOMBWA KUCHUNGUZA MALALAMIKO YA RUSHWA 

TAKUKURU YAOMBWA KUCHUNGUZA MALALAMIKO YA RUSHWA 

0

Na Lydia Churi- Mahakama 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-Takukuru kuyafanyia uchunguzi wa kina malalamiko ya rushwa wanayopokea kutoka kwa wananchi.

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ludewa alipomtembelea Mkuu wa Wilaya hiyo, Bwn. Andrea Tsere ofisini kwake, Jaji Mkuu ameiomba  Takukuru kuyafanyia uchunguzi malalamiko hayo ili kubaini kama yanatokana na wananchi kutofahamu taratibu za Mahakama au ni tuhuma kweli za rushwa.

“Takukuru tunawashukuru kwa kuwa mmetupa ramani ya maeneo yenye viashiria vya rushwa lakini sasa tunawaomba muende hatua ya pili ya kuyachunguza malalamiko yanayoletwa kwenu ili kujua kama yanatokana na wananchi kutokujua taratibu au ni malalamiko ya kweli”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema hatua ya Takukuru kuyachunguza malalamiko hayo itairahisishia Mahakama ya Tanzania kufahamu idadi ya wananchi wasiofahamu taratibu za Mahakama pamoja na kujua kiwango halisi cha vitendo vya rushwa ndani ya Mahakama.

Akizungumzia changamoto za utoaji haki nchini, Jaji Mkuu alisema Mihimili yote mitatu ya dola haina budi kushirikiana kwa karibu kwa kuwa wote wana lengo moja la kumhudumia mwananchi. Aliongeza kuwa huduma za mahakama zinatakiwa kusogezwa karibu zaidi na wananchi kwa ushirikiano wa mihimili yote. 

Alisema changamoto katika kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi bado ni kubwa na hasa kufikisha haki katika ngazi za chini zikiwemo Mahakama za Mwanzo na za wilaya.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania imeandaa Mpango wa miaka mitano unaotoa picha ya maeneo yanayohitaji huduma za Mahakama. Alisema, Mpango huo utaisaidia Mahakama kujipima katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

“Kuanzia sasa mpaka ifikapo mwaka 2020 tunataka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu pamoja na Mahakama za Mwanzo katika kila tarafa nchini”, alisema.

Aliongeza kuwa Mahakama imeshaandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa majengo yake na endapo kutakuwa na wilaya yenye fedha za ujenzi, Mahakama itashirikiana nayo kujenga. 

Akizungumzia utovu wa maadili, Jaji Mkuu alisema Mahakama haifichi changamoto hiyo na katika kupambana nayo, tayari imesambaza mabango ya kupambana rushwa nchi nzima ili kuimarisha Imani ya wananchi kwa mhimili huo. “Bila kuwa na Imani ya wananchi Mahakama hazitakuwa na maana”, alisema.

Kuhusu uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati, Jaji Mkuu alisema taratibu za Mahakama hazina budi kuangaliwa upya kwa kuwa baadhi ni ndefu na haziendani na kasi ya ukuaji wa uchumi huku akitolea mfano wa mashauri ya ardhi na yale ya Mirathi kuwa huchukua muda mrefu na mwisho wake thamani ya mali husika hupotea. 

Aliwataka Majaji na Mahakimu kuifahamu jamii inayowazunguka na kuhakikisha wanamaliza mashauri mapema ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi.