Maafisa kutoka PURA wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Songo Songo iliyopo Kata ya Songo Songo Halmashauri ya Kilwa
Mjiolojia Ebeneza Mollel kutoka PURA akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Songo Songo kuhusu PURA na Mkondo wa Juu wa Petroli kufuatia ziara waliyoifanya shuleni hapo
***********************
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imefanya ziara katika shule ya Sekondari Songo Songo iliyopo Kata ya Songo Songo Mkoani Lindi kwa lengo la kutoa uelewa wa masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia. Ziara hiyo ilifanyika tarehe 19 Februari, 2022 na kuhusisha zaidi ya wanafunzi 50 wa kidato cha pili na kidato cha nne wa shule hiyo.
Mbali na wanafunzi hao, tukio hilo lilihudhuriwa na maafisa wawili kutoka PURA (Bi. Latifa Nyembo ambaye ni Afisa Mazingira na Bw. Ebeneza Mollel – Mjiolojia); Makamu Mkuu wa Shule ya Songo Songo (Bw. Adam Y. Bao); na walimu wengine waliokuwepo shuleni hapo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Ebeneza Mollel alieleza kuwa PURA imekuwa ikifikia makundi mbalimbali kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu Taasisi hiyo na masuala ya mkondo wa juu wa petroli. “Tumefurahi sana siku ya leo kukutana nanyi wanafunzi wa Songo Songo Sekondari. Hii ni mara ya kwanza tunafanya hivi kama Taasisi na kwa kuwa huu ndio mwanzo, ni matumaini yetu tutaendelea kufanya ziara za mara kwa mara ili kuweza kuzungumza nanyi kuhusiana na masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia” aliendelea Bw. Mollel.
Katika hatua nyingine, Bi. Latifa Nyembo aliwahimiza wanafunzi hao kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa ndio msingi wa kada kuu zinazohitajika katika mkondo wa juu wa petroli. “Kwanza nianze kwa kusema masomo yote yana umuhimu na muweke juhudi katika kuyasoma. Aidha, nipende kuwasisitiza kuwa masomo ya sayansi ni muhimu sana katika tasnia ya mafuta na gesi asilia hiyo msiyakimbie. Ni masomo kama masomo mengine na wala hayana ugumu kama ambavyo tumekuwa tukiaminishwa. Kila kitu kinawezekana ukitia juhudi.” alisisitiza Bi. Latifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Adam alisema amefarijika sana kwa ujio wa PURA shuleni hapo kwa kuwa wanafunzi na walimu wa shule hiyo hawakuwa wakifahamu kama kuna Taasisi inaitwa PURA na kazi inazozifanya. Mwalimu huyo pia aliishukuru PURA kwa elimu ya mafuta na gesi asilia kwani ingawa gesi asilia inazalishwa Kijijini hapo bado uelewa wa rasilimali hiyo ni mdogo hususani kwa wanafunzi.
PURA imeendelea kuwafikia wadau mbalimbali kutekeleza matakwa ya Sheria ya Petroli, 2015 na Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta Ndogo ya Petroli za mwaka 2017 zinazoitaka PURA kutoa uelewa wa masuala ya mkondo wa juu wa petroli kwa wadau na jamii kwa ujumla. Hadi sasa PURA imeshafikia makundi anuai yakiwemo ya wafanyabiashara; watoa huduma na wagavi wa bidhaa; waandishi wa habari na wahariri; na watu wenye mahitaji maalumu.