Mfamasia kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando akitoa mafunzo kuhusu njia bora ya kujikinga na kudhibiti maambukizi wakati wa kumuhudumia mgonjwa kwa kufuata taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC guideline).
Afisa kutoka Kitengo cha Uhakika Ubora wa Huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Radenta Bahegwa akijibu hoja kutoka kwa moja ya washiriki wa Semina ya mafunzo juu ya njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti maambukizi kwa kufuata taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC guideline).
Afisa kutoka Kitengo cha Uhakika Ubora wa Huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Radenta Bahegwa akielekeza jambo wakati wa Semina ya mafunzo juu ya njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti maambukizi kwa kufuata kanuni, miiko na taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC guideline).
Picha ya pamoja ikiongozwa na Maafisa kutoka Kitengo cha Uhakika Ubora wa Huduma Wizara ya Afya na Timu ya Wataalamu wa Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) wakati wa Semina ya mafunzo juu ya njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti maambukizi kwa taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC guideline).
*****************
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW-KAGERA
Asilimia 56 ya vifo vya watoto wachanga husababishwa na magonjwa yanayotokea wakati wa utoaji huduma za Afya (Healthcare Associated Infections) katika nchi zinazoendelea.
Hayo yamesemwa na Afisa kutoka kitengo cha uhakiki ubora wa huduma kutoka Wizara Afya Dkt. Radenta Bahegwa kwenye semina ya mafunzo ya njia bora ya namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa (Maambukizi) kwa kufuata kanuni, miiko na taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa IPC Guidline)
Alisema taarifa ya tafiti inasema kuwa 75% ya vifo hivyo vilitokea katika nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo nchi ya Tanzania, huku ukosefu wa huduma ya maji safi yakutosha katika baadhi ya zahanati ikionekana ni moja ya changamoto iliyosababisha tatizo hilo la vifo.
“Tafiti zinaonesha kuwa, 42% ya Vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyo na wodi za kujifungulia havikuwa na maji na vifaa kwaajili ya kuoshea mikono, hali inayopelekea kuwa katika hatari yakupata maambukizi kwa vichanga, mama zao au Watoa huduma”.
Aidha, alisema kutofuata kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa wagonjwa kwa baadhi ya Watoa huduma ni moja kati ya visababishi vikubwa vya vifo vya vichanga vingi katika nchi zinazoendelea, jambo linalorudisha nyuma maendeleo ya Sekta ya Afya katika nchi hizo ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Watoa Huduma kufuata misingi na taratibu za kutoa huduma kwa Wagonjwa (IPC Standard) ikiwemo kunawa mikono ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi yanayotokea wakati wa utoaji huduma kwa Wagonjwa ikiwemo vichanga (Healthcare Associated Infections).
“Usafi wa mazingira kwa kufuata kanuni za usafi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya, hauishii kusafisha maeneo tu, bali hata kupangilia kila kitu ili kikae katika eneo linalostahili”. Alisema Dkt. Radenta Bahegwa.
Aliongeza kuwa kuweka mazingira safi kutasaidia kupunguza hatari za maambukizi kwa Mgonjwa au kwa Watoa huduma, pia kunaongeza hamasa ya kufanya kazi kwa bidi kwa Watoa huduma na kuvutia wagonjwa jambo litalosaidia kuongeza mapato katika Kituo cha Afya.
Kwa upande wake Afisa Afya, Mazingira kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali (JBHN) Bw. Said Chibwana alisema kuwa, Lazima kuwe na choo angalau kimoja kwa kila watumiaji 20 kwa wagonjwa wa ndani, na watumiaji wote 25 kwa Wagonjwa wa nje.
Alisema upatikanaji wa huduma za maji safi katika Vituo vya kutolea huduma za Afya husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia maambukizi ya ugonjwa, kulinda Afya za watoa huduma na Wagonjwa wakati wa utoaji wa huduma za Afya
Wizara ya afya inafanya mafunzo kwa Watoa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) katka Mkoa wa Kagera, lengo ni kuelekeza njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti maambukizi kwa kufuata taratibu na miongozo ya utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC Guideline).