Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Fredy Mwakibete kushoto akimsikiliza Kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania TMA Dk. Agness Kijazi wakati alipotembelea katika mamlaka hiyo.
……………………………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) ametoa rai kwa watanzania kutumia vizuri taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuwa taarifa hizo ni za uhakika. Mhe. Mwakibete, alizungumza hayo wakati wa ziara ya kutembelea Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 28/01/2022.
“kwa niaba ya Serikali na watanzania wengine na mimi binafsi, na kwa niaba ya waziri wangu mwenye kubeba dhamana ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Prof. Mbarawa, niwapongeze sana kwani taarifa zenu zimekuwa za uhakika na ni za kweli”. Alisema. Mhe. Mwakibete.
“Ni rai yangu kwa taasisi zingine na wizara zingine tutumie kikamilifu taarifa zinazotoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, kwa namna hiyo tutakuwa tunaokoa hasara zilizo mbele yetu na kujipanga”. Aliongezea Mhe. Mwakibete.
Akizungumzia suala la changamoto ya maslahi duni, mhe. Waziri alisema kuwa atalisimamia suala hilo kwa kumshirikisha waziri mwenye dhamana na Mamlaka zingine ili kuona namna gani litashughulikiwa ili kuhakikisha wataalamu bingwa wa TMA hawahamia taasisi nyingine.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwakibete alisema, Serikali inatambua umuhimu wa TMA nchini, hivyo Mhe. Rais. Samia Suluhu Hassan kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, ametenga jumla ya Tsh. Bil. 30 ili kukamilisha mtandao wa rada saba nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni taasisi ya Muungano iliyoanzishwa kwa sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ikifanya kazi zake Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar chini ya usimamizi wa Bodi ya TMA (Governing Board).
“Bodi ina jumla ya wajumbe 8, Mwenyekiti na Makamu ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mwenyekiti anatokea Tanzania Bara na Makamu wake anatokea Tanzania Zanzibar, Wajumbe wengine watano (5) wa Bodi ni wateule wa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya hali ya hewa ambapo Katibu wa Bodi hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka. Hawa wajumbe wanawakilisha sekta muhimu zinazotumia taarifa za hali ya hewa”. Alisema Dkt. Nyenzi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alifafanua kuwa Mamlaka imejiwekea malengo yanayolenga kutoa huduma bora zaidi na mahsusi kwa wadau na jamii ili kuchangia katika kutoa maamuzi na hatimaye kuleta maendeleo endelevu.
“Katika kutimiza azma ya Mhe. Rais ya kuwatumikia Watanzania na kutekeleza mipango ya Nchi yetu na ile ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya utoaji wa huduma bora za hali ya hewa nchini, Mamlaka imejipanga kuboresha huduma za hali ya hewa na kuendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini. Aidha mafunzo kwa wafanyakazi na uboreshaji wa mifumo ya menejimenti ya rasilimali fedha itaboreshwa zaidi. Katika kuongeza ubora wa huduma za hali ya hewa, Mamlaka imejiwekea malengo ya kushiriki na kuchangia katika shughuli za hali ya hewa za kitaifa, kikanda na kimataifa hususani katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)”. Alieleza Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi aliishukuru serikali kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kuwa na vitendea kazi vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi ikiwa ni pamoja na kuipatia TMA Rada nyingine mbili ambazo ukamilikaji wake utapelekea kufikiwa kwa malengo ya muda mrefu ya kuwa na Rada 7 za hali ya hewa kwa nchi nzima.