Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli,akizungumza na wachezaji wa TAMISEMI QUEENS kabla ya kuwaaga kwenda kushiriki ligi ya mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza kesho Januari 29, 2022 visiwani Zanzibar.
WACHEZAJI wa TAMISEMI QUEENS wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli (hayupo pichani) wakati wakiagwa kwenda kushiriki ligi ya mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza kesho Januari 29, 2022 visiwani Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli,akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa TAMISEMI QUEENS mara baada ya kuwaaga kwenda kushiriki ligi ya mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza kesho Januari 29, 2022 visiwani Zanzibar.
………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WACHEZAJI wa timu ya TAMISEMI QUEENS wametakiwa kuing’arisha TAMISEMI katika michuano ya ligi ya netiboli ya Muungano huku wakitakiwa kuzingatia nidhamu wakati wote.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 28,2022 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Gelard Mweli wakati akiwaaga kuelekea Zanzibar kushiriki ligi mpira wa netiboli ya Muungano inayotarajia kuanza kesho Januari 29, 2022 .
Mweli amesema kuwa, nidhamu ndio msingi wa mafanikio katika michezo hivyo amewataka wachezaji hao kuiwakilisha vyema Ofisi ya Rais –TAMISEMI katika nidhamu na ushindi.
“Najua kombe tutachukua sababu sisi ni washindi kila siku ila zingatieni nidhamu na uadilifu katika kipindi chote cha michuano, mkumbuke mnaiwakilisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI, tunataka tusikie TAMISEMI Queens sio kwamba inacheza vizuri tu lakini pia kwa nidhamu inaongoza, nidhamu ni sehemu ya ushindi” amesema Mweli.
Aidha, ameupongeza uongozi wa TAMISEMI Sports Club kwa kujituma na kuwekeza muda wao ili kuhakikisha timu hiyo inapata mahitaji yote muhimu katika ligi zilizopita na kuwataka kuendeleza ari hiyo ili mafanikio hayo yawe endelevu.
“Niwapongeze viongozi mnaosimamia timu hii, mnajitoa sana nimeona katika ligi zilizopita umoja wenu na kujituma kwenu kumeleta matokeo mazuri katika timu yetu, niwaombe muendeleze ari hiyo”
amesema Mweli
Pia amewahakikishia wachezaji wa Tamisemi Queens kuwa uongozi wa Tamisemi unatambua jitihada zao katika michezo na wapo tayari kuhakikisha timu hiyo inafikia malengo walio jipangia.
Naye Timu Kapteni Dafroza Luhwago ameushukuru uongozi wa Tamisemi kwa kuhakikisha timu hiyo inakuwa bora kwenye malezi ya kinidhamu na uchezaji pia ameahidi watarudi na ushindi.